Hofu Ebola ikichacha Uganda

Hofu Ebola ikichacha Uganda

NA AFP

KAMPALA, UGANDA

VISA vingine sita vya maambukizi ya Ebola vimegunduliwa nchini Uganda, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilisema Alhamisi jioni.

Hii ni baada ya mtu mmoja kuaga dunia kutokana na maradhi hayo hatari siku ya Jumatano.

Mnamo Jumanne, Wizara ya Afya nchini Uganda ilitangaza mkurupuko wa Ebola katika eneo la kati la mji wa Mubende.

Siku moja baadaye ilithibitisha kifo cha mwanamume mwenye umri wa miaka 24 baada yake kupatikana na virusi Ebola.

“Kufikia sasa tumethibitisha visa saba ambapo mgonjwa mmoja aliyekufa. Watu hao waliambukizwa kirusi cha Ebola,” WHO ilisema kwenye taarifa.

“Watu 40 waliotangamana na wagonjwa hao wametambuliwa na 10 kati yao wanapokea matibabu katika hospitali ya rufaa mjini Mubende,” taarifa iliongeza.

“Tayari wataalamu wetu wamewasili eneo husika kuchunguza hali na kutoa hamasisho kwa umma,” akasema Abdou Salam Gueye, ambaye ni mkurugenzi wa WHO anayesimamia ofisi ya masuala ya dharura barani Afrika.

Uganda, ambayo inapakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imeshuhudia mikurupuko kadha ya Ebola katika miaka ya hapo nyuma.

Mnamo 2019 watu watano walikufa kutokana na ugonjwa huo. Mwezi jana, DRC ilitangaza kisa kimoja cha maradhi hayo katika eneo la mashariki, linalokumbwa na mapigano.

Kisa hicho kiligunduliwa wiki sita baada ya DRC kutangaza kuwa Ebola imetokomezwa kabisa kaskazini magharibi mwa taifa hilo.

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kupanda kwa joto mwilini na kutokwa damu sehemu mbalimbali za mwili. Aidha, mgonjwa hutapika na kuhara.

Kulingana na uchunguzi uliofanywa na WHO, Ebola ni hatari na husababisha maafa haraka mno endapo mgonjwa hatapewa matibabu.Ugonjwa huo uligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini DRC mnamo 1976.

Wataalamu walihoji kuwa ulisababishwa na virusi ambavyo wakati huo viliishi ndani ya mnyama wa porini – popo.

Tangu wakati huo, mikurupuko mingine ya Ebola imeshuhudiwa barani Afrika; kwa jumla imesababisha vifo vya takriban watu 15,000.

Ni vigumu kudhibiti janga la Ebola hasa katika mitaa ya mabanda mijini ambako kuna idadi kubwa ya wakazi.

Watu walio na virusi hawawezi kuambukizwa wengine hadi pale dalili zitaanza kuonekana; hii ikiwa ni baada ya kipindi cha siku 21.

Wakati huu, hakuna dawa kamili iliyoidhinishwa kutibu maradhi ya Ebola.

Hata hivyo, aina kadhaa za dawa zimekuwa zikifanyiwa majaribio nchini DRC na katika baadhi ya mataifa jirani.Mkurupuko mbaya zaidi wa Ebola ulitokea katika mataifa kadha ya Afrika Magharibi kati ya mwaka 2013 na 2016.

Wimbi hilo lilisababisha vifo vya zaidi ya watu 11,300.

Taifa la DRC limeshuhudia mawimbi zaidi ya 10 kufikia sasa. Baya zaidi lilitokea mwaka 2020 ambapo zaidi ya watu 2,280 waliaga dunia.

  • Tags

You can share this post!

Vinono bungeni vyapasua ODM

CHARLES WASONGA: Kuzimwa kwa mawaziri wanaoondoka kutazuia...

T L