Habari

Hofu feri ikitoboka chini

October 29th, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

FERI iliyosababisha kuzama kwa gari na kufariki kwa mwanamke na bintiye wiki chache zilizopita, mnamo Jumapili ililazimika kusitisha shughuli baada ya kugunduliwa ilikuwa na shimo lililokuwa likiingiza maji.

Feri hiyo ya MV Harambee ndiyo iliyosababisha kufa maji kwa Mariam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu mnamo Septemba 29, baada ya gari lao kuteleza na kuingia baharini kutokana na milango ya feri hiyo kukosa kufanya kazi.

Feri hiyo imekuwa katika hali mbaya licha ya mamilioni ya pesa kutumika kuirekebisha.

Ripoti zilisema ilibidi nahodha wa feri hiyo kuiegesha upande wa Likoni kwa ajili ya usalama wa abiria alipogundua kulikuwa na shimo.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa KFS, Bakari Gowa alikanusha kuwa feri hilo ilikuwa na shimo ambalo lilikuwa linaingiza maji.

Hii ni licha ya afisa mmoja mkuu katika shirika hilo kusisitiza kuwa feri hiyo ilikuwa na shimo, jambo ambalo lilifanya isimame kuhudumu.

Taifa Leo ilipozuru eneo hilo Jumapili jioni iliona feri hiyo imeegeshwa upande wa Likoni.

Kuwepo kwa shimo upande wa chini wa feri kunaruhusu maji kuingia, na iwapo shimo hilo ni kubwa basi maji mengi huweza kuingia na kuweza kupelekea kuzama kwa feri.

Mnamo 2016, serikali ilitumia Sh143.5 milioni kuipeleka kwa kampuni ya African Marine and General Engineering ili kufanyiwa ukarabati na kuiruhusu iweze kuhudumu kwa miaka 10 zaidi.

Hii ni baada ya feri hiyo pamoja na MV Nyayo na MV Kilindini kutajwa kuwa hazifai tena kutumika. KFS pia ilitumia Sh400 milioni kwa ajili ya ukarabati wa feri hiyo na ile ya MV Kilindini.

Licha ya kutumika kwa pesa hizo miaka mitatu iliyopita, hali imeendelea kuwa mbaya kwa feri hizo ambazo kila mara zinakuwa na matatizo ya kimitambo na kulazimika ziondolewe mara kwa mara.

Feri nyingine ambazo zinahudumu katika kivuko hicho cha Likoni kwa sasa ni pamoja na MV Jambo, MV Likoni na MV Kwale.