Habari Mseto

Hofu fidia ya Sh1.76 bilioni itazamisha baadhi ya wavuvi kwenye anasa

June 6th, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

MAAFISA wa kamati inayoshughulikia fidia kwa wavuvi walioathiriwa na ujenzi wa Bandari ya Lamu sasa wanasihi wataalamu wa masuala ya fedha na matumizi kutoa ushauri na mawaidha kwa wanaonufaika na fidia hiyo.

Mapema juma hili, Serikali Kuu kupitia Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) ilianza kuwalipa maelfu ya wavuvi wa Lamu fedha ambazo zimekuwa zikisubiriwa kwa kipindi cha karibu miaka saba sasa.

Mnamo Mei, 2018, Mahakama Kuu mjini Malindi iliamuru jumla ya wavuvi 4,734 wa Lamu kufidiwa Sh1.76 bilioni.

Hii ni baada ya korti hiyo kupata kuwa ujenzi wa Bandari ya Lamu ulisababisha athari kubwa, ikiwemo kuharibu maeneo ambayo yalikuwa yakitegemewa na wavuvi kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Kufikia Jumatano wiki hii, zaidi ya wavuvi 3,000 kati ya 4,734 tayari walikuwa wamepokea pesa zao kwenye akaunti zao za benki.

Mwakilishi wa Jamii ya Wavuvi katika Kamati ya Fidia ya Lapsset ambaye pia ni msemaji wao, Bw Mohamed Somo, alisema kila mara fedha nyingi za fidia zinapotolewa kwa wananchi, wengi wao huishia kuwa fukara baada ya muda mfupi kwani hutumia fedha hizo ovyo.

Bw Somo pia alikiri kupokea malalamishi kutoka kwa wanawake, ambao wanadai tayari wameanza kupigwa chenga na waume zao tangu walipofikiwa na neema ya fidia juma hili.

“Kuna wake kadha, hasa kutoka Lamu Mashariki, ambao wamenifichulia kuwa waume zao wamekuwa waongo. Wanaaga nyumbani kwamba wanaenda baharini kuvua kisha wanasafiri kuja kisiwani Lamu kutoa fedha kwa benki kisiri na kuzitumia kwa starehe zao. Baadhi ya wanaume tayari wamepewa onyo kutorudi nyumbani na wake zao,” akasema Bw Somo.

Aliongeza, “Haitakuwa busara kupokea fedha hizo za fidia na badala ya kuleta maendeleo katika familia na ndoa, eti zinaishia kuzivuruga na kuzisambaratisha kabisa ndoa zetu.”

Kauli yake iliungwa mkono na Khadija Lali, mkazi, aliyetaja visa vya mwaka 2015, ambapo waliofidiwa mamilioni ya fedha baada ya ardhi zao kutwaliwa kwa ujenzi wa Bandari ya Lamu wengi wao kwa sasa wamesalia kuwa fukara.

Kuna waliosemekana walikuwa wakiabiri ndege kutoka uwanja wa ndege wa Manda hadi Malindi au Mombasa kununua na kuchana miraa na muguka na kisha kupanda ndege nyingine kurudi Lamu karibu kila siku.

“Nasikitika kwamba endapo wataalamu wa fedha hawatafikishwa Lamu kuwapokeza mawaidha wavuvi wetu, wengi wataishia kuzifuja hela na umaskini kuendelea. Nawasikitikia hata wanawake wenzangu ambao huenda wakapata presha kwani hawa wanaume wetu wa Lamu kila wanapopokea mabunda ya fedha basi huona ndio wakati mwafaka wa kuongeza idadi ya wake nyumbani,” akasema Bi Lali.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Bw Mohamed Mbwana Shee, alishikilia kuwa njia bora ya kuhakikisha walionufaika na fidia za Lapsset wanatumia fedha hizo kwa njia ifaayo ni kwamba serikali na wadau kwanza wangehakikisha wanawapokeza wanufaika elimu hata kabla ya kufikiwa na manoti hayo.