Habari Mseto

Hofu genge likiteka nyara vijana na kuwasafirisha Libya

June 8th, 2024 2 min read

Na MANASE OTSIALO

VIONGOZI wa kijamii katika Kaunti ya Garissa wameelezea hofu kuhusu kukithiri kwa visa vya utekaji nyara wa vijana na kusafirishwa kwao hadi Libya na mataifa ya Mashariki ya Kati.

Bw Abdirahman Hussein, ambaye ni mzee wa kiukoo katika eneo la Modogashe juzi alielezea kisa cha Machi mwaka huu, ambapo vijana wawili, Shukri Siad Abdullahi na Idris Dubow Sheikhnoor, walitekwa nyara na kusafirishwa hadi nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika.

Kulingana na Hussein, watekaji nyara hao waliitisha ridhaa ya Sh5 milioni ili vijana hao waachiliwe huru.

“Sisi kama wanajamii na kwa usaidizi wa mashirika kadha yasiyo ya kiserikali tulichanga pesa hizo, zilizotumwa kupitia mfumo wa Hawala,” akasema.

Hawala ni mfumo usio rasmi wa kutuma pesa bila kusafirishwa pesa taslimu.

Bw Hussein anasema pesa hizo zilitumwa, na raia mmoja mjini Garissa, hadi kwa kundi la Magafe, jina linalotumika kurejelea genge la wahalifu ambalo huwateka nyara watu na kuwapeleka Libya.

Mzee huyo anaamini kuwa Shukri Siad Abdullahi na Idris Dubow Sheikhnoor waliachiliwa huru lakini ajabu ni kwamba hawajarejea nyumbani.

“Kile tunachojua ni kwamba waliachiliwa huru lakini hawakurejea nyumbani. Ni matumaini yetu kwamba wako hai,” Bw Hussein akaeleza.

Muda mfupi baadaye, vijana wengine wawili tena waliripotiwa kutekwa nyara nchini Libya walipokuwa wakielekea Mashariki ya Kati.

“Siku chache baada ya sisi kulipa ridhaa ili vijana hao wawili, Shukri Siad Abdullahi na Idris Dubow Sheikhnoor, waachiliwe huru, video nyingine iliibuka kutoka Libya, mnamo Aprili, ikionyesha vijana wengine wakiteswa,” Bw Hussein akaeleza.

“Sasa hatujui ni vipi tutapata Sh5 milioni zingine ambazo watekaji nyara hawa wanaitisha. Tunajaribu kuwafikia viongozi na maafisa wa wasamaria wema watusaidie,” akaeleza.

Watekaji nyara hao wanaoaminika kuwa wanachama wa genge la Magafe, bado wanawazuilia vijana wanaoaminika kutoka eneo moja.

Ripoti moja iliyotolewa na Shirika la Kimataifa kuhusu Uhamiaji (IOM) haiorodheshi Kenya miongoni mwa nchi zinazochunguzwa kama asili ya idadi kubwa ya wahamiaji haramu nchini.

Inaaminika kuwa idadi ya wahamiaji hao inazidi 700,000 na wao hushirikiana na walanguzi wa watu.

Idadi kubwa ya wahamiaji hao hutoka nchi za Niger, Egypt, Sudan, Chad na Nigeria.

Hata hivyo, ripoti za awali za asasi za usalama zinasema kuwa baadhi ya Wakenya pia wamekuwa wakiuzwa kama watumwa ilhali wengine waliuawa katika mashambulio baada ya kujiunga na makundi ya kigaidi.

Wengi wao waliingia katika mtego huo baada ya kuahidiwa ajira na maisha mazuri katika mataifa ya Kiarabu.

Wakati wa sherehe za Madaraka Dei katika mji wa Modogashe wiki jana, Bw Hussein alitoa wito kwa wanasiasa wa eneo hilo kuungana kuchanga fedha za ridhaa ili zilitumwe kwa kundi la Magafe waachilie vijana waliowateka nyara.