Habari Mseto

Hofu Githurai kuhusu kubomolewa kwa soko kuu

May 27th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

Hali ya wasiwasi imetanda katika soko la Jubilee, mtaani Githurai 45 Kaunti ya Kiambu kufuatia madai huenda litabomolewa tena.

Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya wafanyabiashara na wachuuzi tuliozungumza nao inasemekana kuna barua ya ilani inayosambaa.

Soko hilo liko pembezoni mwa Thika Super Highway, na mita chache kutoka mpaka wa kaunti ya Nairobi.

Barua hiyo kutoka kwa halmashauri ya kitaifa ya barabara kuu nchini (KeNHA), inasema ubomozi utafanyika kesho, Jumanne Mei 28, 2019.

“KeNHA inadai tumejenga vibanda kwenye ardhi ya barabara. Tumekuwa hapa kwa zaidi ya miaka saba, tukiondolewa tutapelekwa wapi ilhali soko hili ndilo hutuzimbulia riziki?” ametaka kujua Antony Kibui, ambaye ameunda duka la mabati katika soko hilo.

Kulingana na Bw Samson Gitau, anashangaa kwa nini wafurushwe ilhali Rais Uhuru Kenyatta 2017 akifanya kampeni za kutetea kuhifadhi kiti chake awamu ya pili aliahidi kuwa soko hilo litajengwa kwa muundo wa kisasa ili kuimarisha biashara.

“Rais mwenyewe aliahidi kuimarisha hali ya Jubilee Market, kwa nini tufurushwe tena? Tunafanya kazi kwa wasiwasi,” akahoji mchuuzi huyo.

Soko hilo lenye ukubwa wa karibu ekari nne, limesitiri zaidi ya wafanyabiashara na wachuuzi 1,000. Uuzaji wa nguo na bidhaa za kula ndiyo biashara kuu inayoendeshwa humo.

Majira ya usiku, soko hilo hugeuzwa kuwa uga wa mikahawa. “Huhudumu saa 24 kwa siku, maelfu ya watu waliojiajiri kupitia soko hili wataenda wapi?” amelia Bi Jecinta, muuzaji wa nguo.

Pia inasemekana vibanda vya soko la mtaa wa Githurai 44, Nairobi, vilivyoko karibu na Thika Super Highway huenda vikabomolewa.

Si mara ya kwanza Jubilee Market kubomolewa. Agosti mwaka uliopita, 2018, waliagizwa kuondoa vibanda walivyokuwa wamejenga. Mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huo, ubomozi wa vibanda na majengo ulifanyika, chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi.

Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu aliambia wafanyabiashara hao kwamba lilibomolewa ili kujengewa soko la ghorofa nne na lenye egesho la magari la kisasa.

Bw Waititu alisema mradi huo utagharimu kima cha zaidi ya Sh2 bilioni, na kufikia sasa hakuna dalili zinazoonekana kuutekeleza.

Baada ya wafanyabiashara hao kuondolewa, waliruhusiwa kurejea tena bali kwa vibanda na majengo tamba. Vikingi vya kuweka ua la kuzingira soko hilo vilisimamishwa.

Ni katika soko hilo pia mabasi yanayohudumu kati ya mtaa wa Githurai na Nairobi, huegeshwa wakati yakipakia abiria.