Hofu hali ya kiangazi kuibua janga jipya

Hofu hali ya kiangazi kuibua janga jipya

Na ALEX KALAMA

WATAALAMU wa masuala ya hali ya hewa wameonya kuwa janga jipya huenda likakumba maeneo yanayoendelea kushuhudia kiangazi.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa katika Kaunti ya Kilifi, imesema huenda kukashuhudiwa ongezeko la wadudu kama vile viwavi kutokana na viwango vya juu vya joto vinavyoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali.

Mkurugenzi wa idara hiyo katika Kaunti, Bi Getrude Leshamta, alisema joto hutoa mazingara yanayohitajika kwa wadudu hatari kuanguliwa kwa wingi.Akizungumza mjini Kilifi, Bi Leshamta, alisema joto linaloendelea kushuhudiwa limechangiwa na kuchelewa kwa mvua za vuli mwanzoni mwa mwezi wa Novemba.

“Kando na ukame, tunatarajia pia viwango vya joto vitachangia uzalishaji wa viwavi, wadudu na ongezeko la magonjwa,’ akasema.Idara ya utabiri wa hali ya hewa ilikuwa imetabiri kuwa mvua ingeanza kunyesha maeneo ya Pwani mwezi huu wa Novemba.

Hata hivyo, kufikia jana, ilikuwa bado kuna jua kali na joto tele.Tahadhari hii ilitolewa huku kukiwa na wasiwasi miongoni mwa wakulima nchini, baada ya nzige waliotatiza uzalishaji chakula mwaka uliopita, kuonekana wakianza kuingia tena nchini.

Juhudi za serikali na mashirika ya kimataifa kuangamiza nzige nchini zilifanikiwa, ila walionekana upya Mandera wiki iliyopita, wakiaminika kutoka nchi jirani kama vile Somalia ambapo ukosefu wa usalama ulitatiza juhudi za kuwaangamiza.

Licha ya hali hiyo, Bi Leshamta, aliwashauri wakulima wajiandae kuhifadhi maji katika mashamba yao kwa kuhakikisha wanatumia mbolea ya samadi ili kuepuka au kuepusha mchanga kukauka haraka huku akiwashauri kupanda miti kwa wingi.

“Kwa hivyo, ninawashauri wakulima wahifadhi kwanza ule mchanga pale katika shamba lao. Watumie mbolea ya samadi ambayo ni mbolea ya kinyesi cha ng’ombe ama cha mbuzi ama cha kuku. Watumie hiyo kwa sababu inasaidia kuzuia yale maji yasiishe kwa urahisi,” akasema.

Wakati huo huo, alisema kuwa iwapo serikali ya Kaunti hiyo kupitia kwa idara ya kilimo itawajibikia suala la uchimbaji visima na mabwawa, basi wakazi hawatakumbwa tena na uhaba wa chakula kwani watakuwa na fursa nzuri ya kupanda mimea mbalimbali kupitia kilimo cha kunyunyizia maji mashambani.

Afisa huyo pia alisisitiza haja ya serikali ya Kaunti hiyo kutenga fedha maalum kuhakikisha wakulima wanawezeshwa na kuhamasishwa kuhusu mbinu mpya za kilimo ili kujiimarisha kimaisha na kuboresha kilimo eneo hilo.

“Kukosekana kwa hamasa kwa wakulima kutoka kwa wataalamu wa kilimo kumewafanya wengi kukosa kunufaika. Hata nawasihi wakulima waache kutegemea ukulima wa mahindi pekee na badala yake wapande mimea mingine ambayo pia ina uwezo wa kustahimili kiangazi.”

You can share this post!

CHARLES WASONGA: KEMSA yadai wafanyakazi wa chini wasifutwe...

Mbunge ajitetea kuhusu matumizi ya fedha za NG-CDF

T L