Habari Mseto

Hofu HIV kuongezeka wakazi kukataa kondomu

September 23rd, 2019 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imeeleza hofu kuhusu idadi kubwa ya wakazi na wageni ambao hawapendi kutumia mipira ya kondomu wanaposhiriki mapenzi.

Ripoti kutoka kwa Wizara ya Afya ya Umma katika kaunti hiyo ilibainisha wengi pia huwa hawataki kupimwa kama wameambukizwa virusi vya HIV, licha ya eneo hilo kurekodi ongezeko la maambukizi ya maradhi hayo katika siku za hivi karibuni.

Licha serikali ya kaunti kujitahidi na kusambaza mipira hiyo kila mwezi, imebainika kuwa ni asilimia ndogo ya wakazi, wageni na hata watalii wa nchi za nje wanaotumia kondomu wakati wanaposhiriki ngono.

Utafiti uliotekelezwa na Kamati Maalum inayohusika na Tathmini ya Mambukizi ya Virusi vya HIV na Ukimwi, Kaunti ya Lamu ulifichua kuwa ni asilimia 40 pekee ya wakazi ambao hutumia kondomu ilhali asilimia 60 ya wakazi hao wakipendelea kufanya mapenzi bila kinga.

Kwa mujibu wa Afisa Mshirikishi wa Virusi vya HIV na Ukimwi, Kaunti ya Lamu, Bw Haji Shibu, kati ya watu 100 wapatikanao Lamu, 3 kati yao wanaishi na virusi vya HIV na Ukimwi, kiwango ambacho alisema kimeongezeka kwa takriban maradufu ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita.

Kulingana na sensa ya mwaka 2009, Lamu iko na jumla ya watu 101,539. Bw Shibu alisema kufikia sasa zaidi ya watu 2,600 tayari wanaishi na virusi vya HIV na Ukimwi kote Lamu.

Baadhi ya maeneo ambayo afisa huyo aliyataja kuongoza kwa maambukizi ya juu ya virusi vya HIV na Ukimwi ni tarafa za Hindi, Amu na Mpeketoni.

Bw Shibu alisema mikakati kabambe inaendelea kote Lamu ili kuona kwamba kiwango hicho cha maambukizi kinashuka siku zijazo.

Alisema kamati yake kwa ushirikiano na idara ya Afya ya Umma Kaunti ya Lamu tayari imesambaza zaidi ya kondomu 15,000 katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita japo matumizi ya mipira hiyo ni finyu kufikia sasa.

Alisisitiza kati ya mwaka 2015 na 2017, kiwango cha maambukizi ya HIV na Ukimwi kote Lamu kilikuwa kati ya asilimia 1.6 na asilimia 2.6 kabla ya kiwango hicho kupanda ghafla hadi asilimia 3 kufikia mwishoni mwa mwaka 2018.

Alisema kamati yake tayari inaendeleza kampeni kabambe kwenye maeneo mbalimbali ya Lamu kuhamasisha wakazi kujiepusha na kushiriki ngono kiholela na pia kuwahimiza kutumia kinga.

Afisa huyo pia alifichua kuwa wakazi wengi wa Lamu hawako tayari kujua hali yao ya virusi vya HIV na Ukimwi, hatua ambayo aliitaja kuchangiwa na unyanyapaa hasa miongoni mwa wanaoishi na maradhi hayo eneo hilo.

Hata hivyo, aliwahimiza wakazi kujitokeza kwenye vituo mbalimbali kupima na kujua hali yao badala ya kuishi gizani.

Ripoti hiyo inajiri wakati ambapo idara ya usalama, Kaunti ya Lamu tayari imewatahadharisha wakazi wa maeneo kunakojengwa miradi mikuu, ikiwemo ule wa Bandari ya Lamu ulioko tarafa ya Hindi na ujenzi wa barabara ya Lamu-Garsen unaopakana na miji ya Mokowe, Hindi, Mkunumbi, Koreni, Kibaoni, Pangani na Witu kujiepusha na makahaba kutoka sehemu zingine za nchi.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, alisema ongezeko la watu wanaofanya vibarua kwenye miradi hiyo na pia ujio wa makahaba eneo hilo huenda ukachangia pakubwa kupanda kwa maambukizi ya maradhi mabaya, ikiwemo HIV na Ukimwi.