Michezo

Hofu IAAF ikipanga kuondoa baadhi ya mbio za Diamond

October 24th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WANARIADHA wa Kenya watapoteza kiasi kikubwa cha posho kwenye mbio za Diamond League, iwapo Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF), litatekeleza pendekezo la kushirikisha fani 12 pekee kwenye kivumbi hicho kuanza msimu ujao.

Mapema mwaka 2019 mataifa ya Kenya na Ethiopia ambayo ni ngome ya watimkaji mahiri katika mbio za masafa marefu yalipinga pendekezo la IAAF kuondoa fani za mbio za mita 5,000 na mita 10,000 kwenye duru za Diamond League.

Mnamo Jumanne wiki hii, Kamati Kuu ya Diamond League ilitangaza kwamba huenda wasimamizi wa mbio hizo wakapunguza fani za msimu huu hadi 12 au 11 pekee kutokana na ufupi wa muda uliopo katika kalenda ya riadha za muhula ujao.

Isitoshe, IAAF ilisisitiza haja ya kujadiliwa kwa idadi ya fani na mbio zitakazopeperushwa moja kwa moja katika kampeni zijazo za Diamond League. Kulingana na IAAF, maamuzi ya mwisho kuhusu jinsi kivumbi cha Diamond League kitakavyoendeshwa mwakani yatatangazwa rasmi mapema mwezi ujao.

Kulingana na ripoti ya awali ya Kamati ya Diamond League, idadi ya fani katika mbio hizo ilipendekezwa kupunguzwa kutoka 32 hadi 24, 12 zikiwa kwa upande wa wanaume na idadi sawa na hiyo kwa upande wa wanawake.

Ripoti hiyo ilipendekeza kwamba mbio ndefu zaidi zitakazoshirikishwa katika kampeni za Diamond League kuanzia mwakani ni zile za mita 3,000 kuruka viunzi na maji.

Kuondolewa kwa mbio za mita 5,000 na mita 10,000 kutakuwa pigo kubwa kwa wanariadha wa Kenya na Ethiopia ambao wamezitawala fani hizo kwa kipindi kirefu.

“Mpangilio mpya wa Diamond League utawaathiri pakubwa wanariadha wazawa wa Afrika ambao sasa watakosa kushiriki baadhi ya mbio ambazo kihistoria, wamekuwa na mazoea ya kuzitamalaki,” akasema Rais wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), Jackson Tuwei.

IAAF inapendekeza kuanzishwa kwa kivumbi cha siku moja cha Mbio za Dunia za Mabara (World Athletics Continental Tour) zitakazotumiwa kuunga orodha ya viwango bora vya kila taifa kwenye ulingo wa riadha kuanzia mwaka wa 2020.

Mwaka ujao utakuwa wa shughuli tele kwa wanariadha wa Kenya watakaopania kushiriki duru 14 za Diamond League ambazo zimeratibiwa kuanza Aprili badala ya Mei jinsi ambavyo imekuwa hapo awali.

Mbali na kivumbi hicho, Wakenya wanapigiwa upatu wa kutamalaki pia Mbio za Nyika barani Afrika, Riadha za Afrika, Mbio za Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 zitakazoandaliwa jijini Nairobi na Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan.