Hofu idadi ya visa vipya vya Covid-19 ikiendelea kupanda

Hofu idadi ya visa vipya vya Covid-19 ikiendelea kupanda

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine idadi ya juu ya maambukizi mapya imerekodiwa Alhamisi.

Kulingana na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe maafisa wake walithibitisha jumla ya visa 829 vipya vya maambukizi ya corona, idadi ya juu zaidi kuandikishwa tangu Januari m2021. Kwa hivyo idadi jumla ya maambukizi nchini tangu mwaka 2020 imetimu 111,185.

Visa hivyo vipya viligunduliwa baada ya sampuli kutoka kwa watu 6,239 kupimwa, hali inayowakilisha kiwango cha maambukizi cha asilimia 13.3.

Kiwango hiki cha juu kimeandikishwa saa chache kabla ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza masharti mapya ya kukabiliana na kuenea kwa corona, masharti ambayo yanatarajiwa kuwa makali zaidi ya yale yanayozingatiwa kwa sasa.

“Nao wagonjwa 91 wamethibitishwa kupona leo (Alhamisi), 47 walikuwa wakitunzwa nyumbani ilhali 44 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali. Kwa sasa idadi jumla ya wale waliopona ni 87,994,” akasema Bw Kagwe.

Idadi ya maafa kutokana na Covid-19 nayo ilipanda hadi 1,899 baada ya mgonjwa mmoja kufariki ndani ya saa 24 zilizopita na hivyo kufikisha idadi jumla ya waliofariki kuwa 1,899.

Kulingana Bw Kagwe kuna jumla ya wagonjwa 566 wa Covid-19 waliolazwa katika hospitali mbalimbali nchini. Wengine 1,694 wako chini ya mpango wa utunzaji nyumbani.

“Nao wagonjwa 91 wamelazwa katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi, 22 wanasaidiwa kupumua kwa mitambo maalum ilhali 60 wameongezewa hewa ya oksijeni,” akaeleza.

Kaunti ya Nairobi inaendelea kuongoza katika idadi ya maambukizi mapya baada ya kuandikisha maambukizi 407 ikifuatwa na Kiambu yenye maambuzki 82.

Kaunti ya Machakos imenakili maambukizi 81, Meru 49, Nakuru 43, Uasin Gishu 26, Busia 20, Embu 18, Mombasa 17 na Kajiado 14.

Visa vingine vipya viliripotiwa katika kaunti zifuatazo; Tharaka Nithi 9, Laikipia 8, Nyandarua 8, Kakamega 7, Kilifi 7, Bungoma 5, Kisumu 5, Homa Bay 4, Murang’a 3, Makueni 3, Kisii 2, Kitui 2, Migori 2, Nandi 2, Nyeri 2, Trans Nzoia 1, Vihiga 1 huku kisa kimoja kikiripotiwa katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.

You can share this post!

Shoo tata ya #WifeMaterial yamtia Eric Omondi matatani

Man-United padogo kuaga Europa League baada ya AC Milan...