Habari Mseto

Hofu jijini magenge yakipora watu mchana

September 3rd, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MAGENGE ya vijana wahalifu yameongezeka katikati mwa jiji la Nairobi mchana na kutia hofu wakazi na wafanyabiashara kwa kuwapora wakiwatisha kwa silaha.

Magenge hayo yana ujasiri wa kupora watu bila kujali kamera za usalama katika maduka na majengo jijini.

Wanawalenga wafanyabiashara na watu wanaotoka kutoa pesa katika benki, mashine za ATM au wanaobeba mikoba wanayoshuku ina bidhaa za thamani kama laptopu.

Tofauti na awali ambapo wahalifu walikuwa wakiendesha shughuli zao maeneo yaliyo na shughuli nyingi hasa kwenye barabara za River Road, Kirinyaga, Luthuli na Ladhies usiku, magenge hayo yamevamia barabara za Kimathi, City Hall, Kenyatta Harambee na University Way ambako yanalenga watu wanaofanya kazi katika ofisi za serikali, mashirika ya kibinafsi na wanafunzi.

“Magenge ya vijana wahalifu walio na bastola na silaha nyingine, wamevamia kati kati mwa jiji mchana na wanawahangaisha watu na wafanyabiashara kwa kuwaibia mali yao. Visa hivi vimeongezeka sana hapa mpaka sisi hatuko salama,” mlinzi mmoja katika barabara ya Moi Avenue aliambia Taifa Leo.

Mlinzi huyo ambaye hatuwezi kutaja jina lake kwa sababu ya usalama wake anasema kwamba haipiti siku mbili kabla ya kushuhudia kisa cha uporaji mchana.

Ingawa Gavana Mike Sonko aliahidi kubuni kikosi cha kukabiliana na wahalifu waliokuwa wakishika watu kabali au ‘ngeta’ jijini Nairobi miaka miwili iliyopita, hali imezidi kuwa mbaya hasa wakati wa miezi minne tangu janga la corona liliporipotiwa nchini.

“Inaonekana magenge yaliyokuwa yakihudumu usiku yamerudi mchana kwa sababu barabara za jiji hazina watu usiku kwa sababu ya kafyu,” alisema mlinzi mwingine kwenye barabara ya City Hall Way.

“Hata mtu akiibiwa, hauwezi ukaona maafisa wa polisi. Ni kama walipelekwa usiku kudumisha kafyu na kuacha wahalifu watawale mchana,” asema mfanyabiashara mmoja ambaye aliibiwa na vijana wanne waliomtambua kwa jina wakimtisha kwa bastola.

Anasema licha ya kupiga ripoti katika kituo cha polisi hakuna hatua zilizochukuliwa.