Hofu kaunti zikiweka dawa zilizopitwa na muda wa matumizi na kuwa sumu

Hofu kaunti zikiweka dawa zilizopitwa na muda wa matumizi na kuwa sumu

Na DAVID MUCHUI

SERIKALI za kaunti zinalaumiwa kwa kuendelea kuhifadhi dawa ambazo muda wa matumizi umepita hali inayohatarisha maisha ya wagonjwa.

Kulingana na Bodi ya Dawa na Sumu (PPB), ni kaunti mbili za Kajiado na Taita Taveta ambazo zimeomba cheti cha kutupa dawa ambazo muda wa matumizi umeisha.

Hospitali zinapaswa kutenga dawa kama hizo kisha kutafuta cheti kutoka PBB ili ziweze kuzitupa kwa njia salama isiyodhuru umma.

Kulingana na Inspekta mkuu wa PPB, Dkt Julius Kaluai licha ya bodi hiyo kuandika barua kwa Baraza la Magavana (CoG) kuhusu suala hilo, kaunti nyingi hazijajibu.

Akiongea katika kikao na wanahabari kuhusiana na msako unaoendeshwa dhidi ya maduka haramu ya dawa katika eneo la Mlima Kenya Mashariki, Dkt Kaluai alisema kuna hatari ya dawa hizo kuuziwa wananchi.

“Serikali za kaunti hazitaki kuwekeza katika mpango wa utupaji wa dawa ambazo muda wa matumizi umeisha kwa sababu ni ghali. Lakini sharti kaunti hizo zifahamu kuwa ni kinyume cha sheria kuendelea kuhifadhi dawa kama hizo,”Dk Kaluai akasema.

Alisema kuwa wakati wa msako huo uliolenga kaunti za Embu, Tharaka Nithi, Meru na Isiolo, wauzaji dawa 46 bandia walikamatwa na maduka 85 ya dawa yaliyokuwa yakihudumu bila kibali kufungwa.

Dkt Kaluai alilalamikia ongezeko la watu kutoka Meru wanaohitimu kutoka vyuo bandia vinavyodai kusomesha kozi za famasia.

“Nyingi ya maduka hayo yanapatikana katika Kaunti ya Meru kwa sababu huko ndiko kuna idadi kubwa ya wataalamu bandia. Wazazi wawe waangalifu na wahakikishe wanawapeleka watoto wao katika vyuo vilivyoidhinishwa. Mtaalamu wa dawa sharti apite mtihani wa PPB kabla ya kupewa cheti cha kuendesha biashara ya dawa,” akasema.

Afisa huyo wa PPB pia aliwaonya wataalamu wa dawa dhidi ya kutumia maelezo yao kusajili maduka ya dawa kisha kuwaachia watu wasiohitimu.

Awali, Dkt Kaluai pia alionya wenye maduka ya jumla ya dawa dhidi ya kuuzia wauzaji rejareja wasiosajiliwa rasmi.

Alisema bodi hiyo imeanzisha mpango wa kushirikisha serikali za kaunti katika kuhakikisha kuwa maduka haramu ya dawa hayapewi leseni za kuendesha biashara hiyo.

“Kuna pendekezo kwamba bodi yetu ifanye kazi na serikali za kaunti kiasi kwamba biashara zilizosajiliwa na PPB ndizo zipewe leseni za biashara. Mpango huo unaendelea,” akaongeza Dkt Kaluai.

  • Tags

You can share this post!

Polisi sasa kumfungulia shtaka mwanamume aliyeua watu 8

Serikali yatakiwa iboreshe soko la utalii humu nchini

T L