Michezo

Hofu Kenya Morans baada ya kocha Cliff Owuor kuyoyomea APR ya Rwanda

November 30th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Cliff Owuor wa timu ya taifa ya wanavikapu wa Kenya Morans amejiunga na kikosi cha Rwanda Patriotic Army (APR).

Owuor hakurejea Kenya wikendi iliyopita pamoja na kikosi na maafisa wengine wa benchi ya kiufundi wa Morans aliosafiri nao jijini Kigali, Rwanda kwa mechi za raundi ya kwanza za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AfroBasket) kati ya Novemba 25-28, 2020.

Chini ya Owuor, Morans walipiga Msumbiji 79-62 katika mchuano wa mwisho wa Kundi B na kuweka hai matumaini ya kufuzu kwa fainali za AfroBasket zitakazoandaliwa Rwanda mwaka 2021.

Wanavikapu wa Morans waliingia ugani dhidi ya Msumbiji wakitawaliwa na kiu ya kushinda baada ya chombo chao kuzamishwa na Senegal (92-54) na Angola (83-66) katika mechi mbili za ufunguzi wa Kundi B.

Iwapo Morans watashinda mechi mbili kati ya tatu za marudiano dhidi ya Angola, Senegal na Msumbiji katika mkondo wa pili mnamo Februari 2021, basi Kenya itafuzu kwa kunogesha fainali za Kombe la Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1993.

Owuor ambaye amewahi kudhibiti mikoba ya APR hapo awali kwa miaka 15 hadi 2018 amesema: “Amekuwa akiwaniwa sana na miamba hao wa vikapu nchini Rwanda tangu Agosti 2020 na alisalia jijini Kigali ili kutathmini ofa ya kikosi hicho kabla ya kurasimisha uteuzi wake hivi karibuni.”

Hata hivyo, Peter Orero ambaye alikuwa mkurugenzi wa kikosi cha Morans kwenye mashindano ya kufuzu kwa AfroBasket jijini Kigali, ametaka Shirikisho la Vikapu la Kenya (KBF) kufanya hima na kumshawishi Owuor kurejea nchini kuendelea na majukumu yake kambini mwa Morans.

Orero ambaye kwa sasa ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Dagoretti, Nairobi, ndiye mwekahazina wa KBF.

Hadi alipopokezwa mikoba ya Morans, Owuor alikuwa akiwatia makali wanavikapu wa Chuo Kikuu cha USIU-A.

Orero ameshikilia kwamba Morans watakuwa na kila sababu ya kutwaa taji la FIBA AfroBasket mwaka ujao nchini Rwanda na kujikatia tiketi ya Kombe la Dunia mnamo 2023 iwapo watapigwa jeki vya kutosha.

“Malengo tuliyojiwekea ni makubwa. Iwapo tutapata msaada wote tunaohitaji na tufanikiwe kushawishi wanavipaku wetu wote mahiri wanaochezea ughaibuni kujumuika nasi kwa kibarua kinachotusubiri kwa wakati, kisha tuendelee kujivunia huduma za Owuor; sioni chochote kingine kitakachotuzuia kunogesha Kombe la Dunia,” akasema.

Kipute cha Vikapu vya Kombe la Dunia kitafanyika nchini Indonesia, Japan na Ufilipino mnamo 2023. Itakuwa mara ya kwanza katika historia kwa mashindano hayo kuandaliwa katika zaidi ya nchi moja.

Kwa Kenya Morans kujikatia tiketi ya kushiriki fainali za FIBA AfroBasket zitakazoandaliwa jijini Kigali, Rwanda mwaka ujao, itawalazimu mwanzo kuambulia nafasi ya pili au kuwa wa kwanza katika Kundi B baada ya marudiano dhidi ya Angola, Senegal na Msumbiji katika mechi za kufuzu mnamo Februari 2021.

Mkondo wa pili ya kipute cha Afro-Basket umeratibiwa kuanza Februari 19, 2021 kwa mechi itakayowakutanisha tena Kenya na Senegal. Baadaye, wanavikapu wa Morans watashuka ugani kukabiliana na Angola mnamo Februari 20 kabla ya kumaliza udhia dhidi ya Msumbiji mnamo Februari 22.

Kwa mujibu wa orodha ya viwango bora vya kimataifa, Morans ndio wanaokamata nafasi ya chini zaidi kwenye Kundi B. Wanashikilia nambari 122 duniani huku Angola, Senegal na Msumbiji wakiwa katika nafasi za 32, 35 na 93 mtawalia.