Habari Mseto

Hofu kijijini baada ya jamaa aliyezikwa 'kufufuka'

September 19th, 2018 1 min read

Na RUSHDIE OUDIA

WAKAZI wa kijiji cha Ung’oma, eneo la Alego Usonga, Kaunti ya Siaya, Jumanne walieleza jinsi walivyoshtushwa na jamaa yao aliyerejea nyumbani Alhamisi iliyopita ilhali walikuwa ‘wamemzika’ Agosti 3.

Bw Charles Odhiambo Ombuga, alirudi nyumbani wiki iliyopita na kushtua jamaa wengi na marafiki zake ambao walikuwa wameanza kutuliza moyo baada ya ‘kifo na mazishi yake’ mwezi uliopita.

Mke wake, Bi Benta Akinyi, alisema hangeweza kutambua mwili alipoambiwa ulikuwa wa mume wake waliyeoana kwa miaka 11, kwani ulikuwa umeharibika sana.

Bw Odhiambo aliwaambia wasiogope kwani hakuwa nyumbani kwa karibu miezi sita ingawa hakuelewa kwa nini familia yake iliamini alikufa.

“Nadhani ni vile hatukuwa tukiwasiliana mara kwa mara,” akasema.

Naibu wa Chifu wa lokesheni ndogo ya Kalkada Uradi, Bw William Ogutu, alisema sasa itabidi mwili uliozikwa ufukuliwe punde agizo la mahakama litakapopatikana kisha matambiko ya kitamaduni yafanywe kutakasa boma hilo pamoja na wote waliohusika katika mazishi.

Bi Margaret Ombunga ambaye ni mamake Bw Odhiambo, alisema walipoenda katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga, walipata mwili waliodhania kuwa wake ukiwa chini ya miili mingine mitatu.

Alisema hangeweza kutambua mwili huo vyema lakini aliona alama kwenye mguu wa kushoto ambayo ilimshawishi kwamba mwili ulikuwa wa mwanake.Familia yake ilidai waliamua kwenda katika hifadhi hiyo baada ya ‘kupokea maono’ kwamba alikuwa amefariki na mwili wake ulikuwa huko.