Jamvi La Siasa

Hofu kuzaana kuongeza kura kutaangusha Mlima Kenya

March 31st, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

KINAYA kimezuka katika eneo la Mlima Kenya ambapo wanasiasa wamezindua mchakato wa kuwataka wenyeji wazaane kwa wingi ilhali wao wenyewe walipanga uzazi na kuishia kuwa na familia ndogo.

Katika misururu ya kampeni ambazo zimezinduliwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye ana watoto wawili, amekuwa akiambia wenyeji wazae kwa kila ndoa zaidi ya watoto saba.

“Hata ikiwezekana zaeni watoto 10. Mimi nilidanganywa na wazungu na nikapata wawili tu. Ninyi vijana hasa tunaookoa kutoka kwa ulevi wa kiholela, zaeni watoto wengi ndio jamii hii yetu isiishe na tubakie na nguvu,” akasema Bw Gachagua katika kijiji cha Kaimbaga kilichoko Kaunti ya Nyandarua mnamo Ijumaa iliyopita.

Bw Gachagua aliwataka wenyeji waelewe kwamba kuzaana kuna umuhimu wake.

Viongozi wengi katika eneo la Mlima Kenya walipanga uzazi ambapo walio na watoto wengi, huwa ni familia ya watoto wanne.

Rais Mstaafu Mwai Kibaki alikuwa na watoto wanne, mwekezaji bilionea marehemu Lizzie Wanyoike akiwa na watatu, shujaa Kenneth Matiba naye akajaliwa watoto watatu.

Kwa sasa, Gavana Irungu Kang’ata ana watoto watatu huku Seneta Joe Nyutu akiwa na watoto watatu.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Anne Waiguru, ambaye ndiye Gavana wa Kirinyaga, ana watoto wawili sawa na kinara wa Narc Kenya Martha Karua.

Wanasiasa wa eneo hilo ambao wamekumbatia kampeni hiyo ya kupigigia debe kuzaana ni pamoja na mbunge wa Maragua Mary wa Maua ambaye ana watoto watatu, mbunge wa Mathioya Edwin Mugo ambaye hajatangaza wake ni wangapi pamoja na Seneta Nyutu aliye na watatu.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth ana wawili.

Hata hivyo, ni bora ieleweke kwamba kuwa na watoto au kutokuwa nao sio kigezo cha uongozi kwa kuwa Mungu ndiye hubariki uwezo wa kuwapata.

Lakini kwa wanasiasa walio na uwezo wa kupata watoto wengi na hawakupata au kuweka mikakati ya kuwapata ndio wanatiliwa shaka kama kampeni zao ni za nia njema dhidi ya wenyeji.

“Hili ni suala nyeti sana ambalo linahusiana na uwezo wa jamii kubakia na ukiritiba wa idadi hasa ya wapigakura na uwezo wa kulea kwa kuafikia haki za kimsingi kwa watoto hao,” asema mshirikishi wa vuguvugu la vijana wa Mlima Kenya Bw Gitau Warui.

Bw Warui anashindwa kuelewa itakuwaje wanasiasa walio na pesa kwa magunia walemewe kuzaa watoto wengi huku wakiwataka maskini katika jamii wazaane kama panya.

Mratibu wa Kitengo cha e-Health katika Wizara ya Afya Dkt Onesmus Mwaura anasema kwamba upangaji uzazi ni kiungo kimoja thabiti cha kuafikia ustawi wa kimaendeleo.

“Upangaji uzazi haumaanishi kuzaa watoto wachache. Humaanisha kuzaa watoto wale ambao hawataathiri vibaya afya ya mama na pia hawataathiri uwezo wa malezi hasa katika kuafikia lishe, afya, mavazi, makazi na elimu bora,” asema Dkt Mwaura.

Anasema kwamba wale walio na uwezo wa kutii wito huo wa wanasiasa wako huru kukimbizana na uzazi lakini wale wasio na uwezo wanafaa tu watulie.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Agikuyu Wachira Kiago anasema kwamba hakuna shida ya kuzaa lakini kuna shida ya malezi.

“Jamii ikipanuka ni jambo la fahari kwetu na ndio sababu tunafaa kutia bidii katika kufufua uchumi wa kijamii ndio watu wawe na uwezo wa kuzaana,” akasema Bw Kiago.

Alisema yeye anaunga mkono familia kubwa kwa walio na uwezo.

“Lakini haina haja tujitose kwa bahari ya umaskini kiholela kupitia kuzaa watoto ambao tutawaacha katika mitaa wakiwa chokoraa,” akasema.

Naye Bw Warui abaongeza kwamba “tusipochunga hapa Mlima Kenya tutawekwa kwa mtego wa sisi wanyonge kuzaa kura tu pamoja na wananchi wa kuitwa kufanya maandamano”.

“Matajiri huku kwetu wanazaa watoto kidogo na kuwapa elimu bora ili waishie kuwa viongozi wetu wa kesho, kitu ambacho hakiko mbali sana na ukoloni wa matajiri wetu kukalia maskini wao,” akasema mshirikishi huyo wa vijana.

[email protected]