Habari Mseto

Hofu Lamu baada ya wafugaji kuona barabarani kifaa kinachofanana na kilipuzi

October 28th, 2019 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

TAHARUKI ilitanda katika eneo la Koreni, tarafa ya Mkunumbi Jumamosi baada ya kifaa kinachofanana na kilipuzi cha kutegwa ardhini kuonekana katikati mwa barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen, karibu na Shule ya Msingi ya Koreni.

Kifaa hicho kiligunduliwa na wafugaji waliokuwa kwenye shughuli zao za kulisha mifugo eneo hilo ambalo ni makazi ya wafugaji wengi wa kuhamahama.

Ililazimu maafisa wa usalama, ikiwemo wale wa jeshi la Kenya (KDF) na polisi kutumwa ghafla eneo hilo ili kubainisha iwapo kifaa hicho kilikuwa kweli ni kilipuzi.

Akithibitisha tukio hilo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia alisema maafisa wa KDF na polisi waliotumwa eneo la tukio walikiondoa kifaa hicho haraka iwezekanavyo na kisha kukiharibu kwa utaratibu salama.

Bw Macharia alisema kifaa hicho kilibainika kuwa kipuri cha mashini na wala hakikuwa kilipuzi wala guruneti kama ilivyokisiwa na wakazi.

Aliwataka wananchi kuondoa shaka, akisisitiza kuwa usalama umedhibitiwa vilivyo kote Lamu.

Pia aliwataka kuendelea kushirikiana kwa karibu na walinda usalama na kupiga ripoti iwapo watashuhudia mtu au tukio lolote ambalo si la kawaida.

“Ilikuwa majira ya saa tatu hivi asubuhi ambapo tulipokea ripoti kutoka kwa raia wema eneo la Koreni, tarafa ya Mkunumbi kwamba kulikuwa na chombo kisichoeleweka kilichokuwa kimetupwa katika barabara ya Lamu-Garsen, karibu na shule ya msingi ya Koreni. Maafisa wetu wa usalama walipofahamishwa walifika mara moja pahala pale bila kukawia, ambapo walikiondoa na kisha kukiharibu chombo hicho. Cha muhimu ni kwamba chombo kilithibitishwa kuwa kipuri cha mashine ambacho kilikuwa kimekaa kwa muda mrefu ardhini na wala sio kilipuzi kama ilivyokisiwa. Wananchi wasiwe na hofu wala kiwewe. Usalama ni dhabiti Kaunti ya Lamu,” akasema Bw Macharia.

Kushukuru

Mmoja wa wafugaji, Bw Hussein Ali aliishukuru idara ya usalama kwa kufika haraka eneo hilo baada ya kufahamishwa kuhusu chombo hicho ambacho tayari kilikuwa kimezua taharuki miongoni mwa wakazi wa Koreni na pia wasafiri wanaotumia barabara ya Lamu-Garsen.

“Barabara tayari ilikuwa haipitiki kwani hofu ilikuwa imetanda miongoni mwa madereva na wasafiri. Sisi wakazi wa Koreni pia tulikuwa na wasiwasi kufuatia kuonekana kwa kifaa hicho. Tunashukuru maafisa wetu wa usalama kwa kufika haraka na kubainisha kuwa chombo hicho hakikuwa na madhara yoyote kwani kilikuwa kipuri tu wala si kilipuzi. Tuko shwari sasa,” akasema Bw Ali.

Eneo la Koreni ni takribani umbali wa kilomita moja kutoka eneo la Milihoi ambapo linafahamika sana kwa visa vya al-Shabaab kutega vilipuzi vya ardhini mara kwa mara, ambapo wamekuwa wakiua walinda usalama na raia.

Hali hiyo iliisukuma serikali kubuni kambi ya polisi wa kukabiliana na ghasia (GSU) ya Milihoi mapema mwaka 2018 hatua ambayo imesababisha mashambulizi ya kigaidi kusitishwa kabisa eneo hilo tangu kambi hiyo ilipobuniwa.

Mbali na Milihoi, serikali pia iliafikia kubuni kambi nyingine za polisi na jeshi kwenye maeneo ya Nyongoro, Mambo Sasa na Lango la Simba ili kudhibiti zaidi usalama wa wasafiri na walinda usalama wanaotumia barabara kuu ya Lamu-Garsen.