Hofu Lamu kufuatia ongezeko la vijana wanaotumia dawa za kulevya

Hofu Lamu kufuatia ongezeko la vijana wanaotumia dawa za kulevya

Na KALUME KAZUNGU

VIONGOZI na wazee, Kaunti ya Lamu wameelezea kutamaushwa kwao na ongezeko la vijana wanaotumia dawa za kulevya eneo hilo.

Wakizungumza na wanahabari, viongozi hao, akiwemo Mbunge wa Lamu Mashariki Athman Sharif na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake eneo hilo Bi Ruweida Obbo, wanasema hawajafurahishwa na jinsi vijana wengi kote Lamu wanavyoendelea kutumia mihadarati.

Bw Sharif alieleza haja ya idara ya usalama eneo hilo kuwasaka na kuwachukulia hatua kali za kisheria wasambazaji wa mihadarati ili wasiendelee kuharibu maisha ya vijana.

“Haipendezi kuona vijana wetu ambao ni nguzo ya kesho wakiendelea kuharibika kwa dawa za kulevya hivyo ni vyema idara ya usalama kujikakamua na kupiga vita hili janga la mihadarati ili kuzuia vijana zaidi kupotelea katika uraibu,” akasema Bw Sharif.

Bi Obbo alisisitiza haja ya idara ya usalama kuwakabili vilivyo wasambazaji na wauzaji wa mihadarati kaunti ya Lamu, ikiwemo kuwapiga risasi na kuwaua.

Alisema jamii ya Lamu haiwezi kujiendeleza ipasavyo ikiwa vijana wataendelea kupotelea kwenye janga la dawa za kulevya.

Bi Obbo aidha aliwataka wazazi kuwapa malezi bora vijana wao ili wasipotoshwe.

“Nimekuwa nikisukuma miswada bungeni kutaka walanguzi wa mihadarati kupewa adhabu kali, ikiwemo kifo. Msimamo wangu ni kwamba watakaopatikana wakisambaza dawa za kulevya Lamu wachukuliwe kama majambazi. Wapigwe risasi papo hapo na kuuawa. Hao pia ni wauaji,” akasema Bi Obbo.

Kwa upande wao, wazee wa Lamu walitaja mihadarati kuwa kisiki kinachozuia idadi ya watu kuongezeka eneo hilo.

Kassim Omar alisema mihadarati imewageuza vijana wa Lamu kuwa mbumbumbu, hivyo kuwazuia kutekeleza majukumu ya kifamilia.

“Wale ambao walikuwa wameoa ndoa zao kwa sasa zimesambaratika hasa baada ya kujitosa kwenye janga la mihadarati. Hawawezi kukimu familia zao, ikiwemo majukumu ya kitandani. Vijana wameacha kuzaa kwa sababu ya kutumia mihadarati na hata kukosa hamu ya mke. Idadi ya watu wa jamii yetu ya Kibajuni ambayo ni ndogo itaongezeka vipi ikiwa hatuzaani? Hili ni suala linalotutia hofu,” akasema Bw Omar.

Ali Shee alisema mihadarati imeongeza uhalifu mitaani kwani makazi ya watu, vioski na maduka yamekuwa yakivunjwa na bidhaa kuibwa na vijana wanaotumia mihadarati.

“Wizi umekithiri mitaani na vichochoroni na yote yanatokana na ulanguzi wa mihadarati. Vijana wetu wanatumia mihadarati na hawana kazi. Hao ndio huvunja nyumba za watu na maduka ili kuiba bidhaa wakauze na kujipatia fedha za kununulia mihadarati. Lazima hali hii ikabiliwe vilivyo kwani inatisha,” akasema Bw Shee.

Wazee hao aidha waliiomba serikali ya kitaifa na ile ya kaunti kuwafadhili vijana walioathiriwa na mihadarati kujiunga na vituo vya kuwarekebisha tabia nchini.

Walisema baadhi ya waathiriwa wa mihadarati wako tayari kujiunga na vituo vya kuwarekebisha tabia ili wawe raia wema lakini familia zao hazina uwezo wa kugharimikia huduma kwenye vituo husika.

You can share this post!

Messi afunga mawili dhidi ya Bilbao na kubeba Barcelona...

Wanaraga wa Shujaa wapangiwa mechi zaidi za kirafiki barani...