Michezo

Hofu Liverpool ikijiandaa kuvaana na Chelsea Super Cup

August 14th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MERSEYSIDE, UINGEREZA

KIPA nambari moja wa Liverpool, Alisson Becker atasalia mkekani kwa kipindi cha “majuma kadhaa” yajayo kuuguza jeraha la mguu alilopata wakati wa mchuano wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya limbukeni Norwich City wiki iliyopita.

Haya ni kwa mujibu wa mkufunzi wake Jurgen Klopp ambaye ameungama kuwa kuumia kwa Alisson huenda kukayumbisha pakubwa uthabiti wa kikosi chake ambacho kinajiandaa leo Jumatano kuvaana na Chelsea katika gozi la Super Cup jijini Istanbul, Uturuki.

Chelsea watashuka dimbani kwa minajili ya mechi hiyo ambayo hukutanisha watetezi wa taji la UEFA na washikilizi wa Europa League, wakipania kujinyanyua baada ya Manchester United kuwapokeza kichapo cha 4-0 katika EPL wikendi jana ugani Old Trafford.

Alisson mwenye umri wa miaka 26, aliondolewa uwanjani kunako dakika ya 39 ya mchezo uliowashuhudia Liverpool wakijivunia ushindi mnono wa 4-1 mbele ya mashabiki wao wa nyumbani ugani Anfield.

Nafasi ya Alisson ambaye ni kipa ghali zaidi duniani kwa sasa ilijazwa na sajili mpya Adrian San Miguel aliyebanduka kambini mwa West Ham United msimu huu na kutua Anfield kuwa kizibo cha Simon Mignolet.

Mignolet aliyekuwa tegemeo la Liverpool hadi Alisson alipojiunga nao kutoka AS Roma mnamo Juni 2018, aliyoyomea Ubelgiji kuvalia jezi za kikosi cha Club Bruges kilichomshawishi kwa Sh830 milioni wiki iliyopita.

Adrian, 32, aliingia katika sajili rasmi ya Liverpool akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na West Ham almaarufu ‘The Hammers’ kutamatika mwishoni mwa msimu jana.

Katika kipindi cha miaka sita ambapo aliwadakia West Ham, Adrian aliwajibishwa mara 150 tangu aliposajiliwa kutoka Real Betis mnamo 2013. Kipa huyu mzawa wa Uhispania anatarajiwa sasa kuchukua nafasi ya Alisson aliyevunja ndoa yake na Roma kwa kima cha Sh8.4 bilioni.

Japo ujio wa Adrian ulimfanya kuwa kipa wa nne wa Liverpool, miamba hao wa soka ya Klabu Bingwa Ulaya wana kila sababu ya kumpanga sasa katika kikosi cha kwanza hasa ikizingatiwa kwamba makinda Sepp van den Berg na Harvey Elliott ambao ni makipa wengine kambini mwao bado hawana tajriba ya kutosha.

“Hali si sawa. Alisson ana jeraha la mishipa ya mguu ambalo litamweka nje kwa muda,” akasema Klopp hapo jana.

Kwa kutofahamu uhakika wa muda ambao Alisson atahitaji kuuguza jeraha, Klopp amedokeza uwezekano wa Liverpool kujinasia maarifa ya kipa veterani Andy Lonergan kwa mkataba wa miezi michache.