Hofu maambukizi ya Covid yakianza kuongezeka tena

Hofu maambukizi ya Covid yakianza kuongezeka tena

Na BENSON MATHEKA

MATUMAINI ya Wakenya kwamba agizo la kutotoka nje usiku litaondolewa hivi karibuni ili warudie shughuli zote za kiuchumi, yameanza kudidimia kufuatia ongezeko la maambukizi mapya ya virusi vya corona.

Mnamo Januari, Rais Uhuru Kenyatta aliongeza muda wa kafyu hadi Machi 12 anapotarajiwa kutoa uamuzi mpya.

Alipoongeza muda huo Januari, Rais Kenyatta aliwataka Wakenya kuendelea kuzingatia kanuni za kuzuia msambao wa virusi hivyo akiahidi kufungua uchumi kikamilifu iwapo Kenya itatimiza viwango vinavyohitajika kimataifa vya chini ya asilimia tano kwa wiki mbili mfululizo kuukabili.

Hata hivyo, alisema kwamba ikiwa maambukizi yataongezeka, hatasita kurejesha hatua kali ili kulinda raia.

Kuanzia wakati huo, kiwango cha maambukizi kimekuwa cha chini hadi wiki mbili zilizopita ambapo idadi ya wanaothibitishwa kuwa na ugonjwa ilipoanza kuongezeka kila siku.

Kuanzia Januari, alipolegeza masharti na kuruhusu biashara kufunguliwa isipokuwa baa na magari ya uchukuzi kutobeba idadi kamili ya abiria, Wakenya walianza kupuuza kanuni za kunawa mikono kila wakati, kuvalia barakoa katika maeneo ya umma na kudumisha umbali kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

Hii ilifuatia hatua ya wanasiasa kuandaa mikutano mikubwa ya kisiasa na kuhudhuria mazishi ambapo huwa watu wanatangamana.

Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe amekuwa akionya Wakenya wasihudhurie mikutano ya wanasiasa kwa usalama wao.

“Ushauri wangu kwa Wakenya ni kuwa virusi hivi vingali katika jamii na la muhimu ni kila mtu kujikinga binafsi. Ukikosa kwenda kwa mikutano ya wanasiasa, hawataandaa mikutano,” Bw Kagwe alisema akihojiwa na kituo kimoja cha redio.

Hata hivyo, viongozi walipuuza ushauri huo jambo ambalo limewafanya raia kuwaiga na kupuuza kanuni za kujikinga dhidi ya corona.

Kwa muda wa wiki mbili sasa, idadi ya maambukizi mapya imekuwa ikiongezeka, tofauti na mwezi Desemba mwaka jana na Januari ambapo ni watu wachache waliokuwa wakithibitishwa kuambukizwa virusi hivyo.

Ijumaa, wizara ya afya ilitangaza kuwa watu 410 waliambukizwa virusi hivyo ndani ya saa 24 baada ya kupima sampuli 7, 180.

Taarifa ya wizara ilisema watu sita walifariki kutokana na maradhi hayo hatari na kufikisha 1,853 waliouawa na virusi hivyo nchini.

Mnamo Jumanne, wizara ilitangaza kwamba watu 10 walifariki kutokana na virusi hivyo.

Shule zilizopofunguliwa Januari mwaka huu, wataalamu wa afya walionya kuwa maambukizi yangeongezeka Machi. Walisema kwamba watu wengi walichukulia kufunguliwa kwa shule kama ishara ya kukabiliwa kwa virusi hivyo nchini na wakaacha kuzingatia kanuni za wizara ya afya za kujikinga na kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.

Wataalamu wa afya wanahofia kwamba huenda hali ikawa mbaya zaidi siku zijazo iwapo aina mpya ya virusi inayogunduliwa katika mataifa ya Afrika Kusini na Uingereza itapenya nchini.

Wanasayansi wa Afrika Kusini wanasema aina hiyo mpya inasambaa kwa haraka na kuua watu wa umri mdogo tofauti na iliyogunduliwa China ambayo ililemea sana watu wa umri mkubwa na walio na matatizo sugu ya kiafya.

You can share this post!

BI TAIFA FEBRUARI 27, 2021

Man-Utd wapewa AC Milan, Arsenal kuvaana na Olympiakos huku...