Habari Mseto

Hofu mahindi yataisha Kenya majuma 3 yajayo

June 2nd, 2019 2 min read

Na BARNABAS BII

KENYA inakodolewa macho na upungufu wa chakula siku chache zijazo, kwani mahindi yanazidi kupungua maghalani huku Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri akisisitiza kuwa hakuna mahindi yatakayonunuliwa kutoka nje ya nchi.

Wataalamu wanadai kuwa mahindi yaliyomo nchini kwa sasa yatakimu nchi kwa wiki tatu, huku mavuno yanayofuata yakitarajiwa kuja baada ya Agosti, kutoka Kusini mwa Bonde la Ufa.

Mavuno hayo, hata hivyo, hayatakuwa ya kuridhisha kutokana na msimu wa kiangazi ambao ulidumu kwa muda mrefu mwaka huu.

Aidha, habari kuhusu kiwango halisi cha mahindi ambacho Bodi ya Uhifadhi wa Nafaka Nchini (NCPB) na kampuni za kusaga mahindi zinahifadhi katika maghala yake kwa sasa hakijulikani.

Maafisa kutoka wizara ya Kilimo waliambia Taifa Leo kuwa NCPB inahifadhi takriban magunia milioni 1.5 ya mahindi, nayo mashirika ya kutengeneza unga zaidi ya magunia 700,000.

Kiwango hiki ni kidogo na kitakimu taifa kwa wiki tatu, ikizingatiwa kuwa Ghala la Vyakula Muhimu (SFR) wiki iliyopita lilitoa magunia 1.7 milioni ya mahindi, na kuuzia kampuni kubwa za kutengeneza unga magunia milioni moja na 700,000 kampuni ndogo, kwa Sh2,300 kwa gunia la kilo 90.

Mashirika hayo, hata hivyo, yametaja kiwango hicho kuwa kidogo na bei ya unga bado haijabadilika.

Kampuni ndogo Ijumaa zilieleza Taifa Leo kuwa zilikuwa zimelipa bodi ya NCPB pesa nyingi lakini sasa zinaamini kuwa huenda bodi hiyo haina mahindi ya kutosha kuwauzia.

Hali imeharibiwa na mzozo baina ya wizara hiyo na NCPB, kuhusu deni la Sh11 bilioni. NCPB inasema kuwa ucheleweshaji wa kulipa umekawisha shughuli zake, huku ikikumbwa na changamoto kama kuchelewesha mishahara ya wafanyakazi kwa miezi miwili iliyopita.

“Kumekuwa na kucheleweshwa kutoa mahindi kwa kampuni za kutengeneza unga lakini tunatarajia kuwa idara hizo mbili zitaafikiana kwa haraka na kupata suluhu,” afisa wa mawasiliano NCPB Titus Maiyo akasema.

Wizara ya Kilimo na SFR zinadaiwa na NCPB Sh8 bilioni na Sh3 bilioni mtawalia, kwa ununuzi wa mbolea na kemikali na magunia ya kuhifadhi mahindi.

Mwenyekiti wa SFR Noah Wekesa, hata hivyo, amekana kuwa bodi yake inadaiwa na NCPB pesa zozote, badala yake akasema inadai malipo kwa mauzo ya mahindi na NCPB.

Vikundi vya mashirika yaliyokuwa yameenda kuchukua mahindi kutoka kwa maghala ya NCPB baada ya kuruhusiwa na SFR walipolipia vilirejeshwa bila mahindi.

“Tulilipia mahindi wiki iliyopita na hivyo wizara ya Kilimo inafaa kutuharakishia zoezi la kutupa mahindi ili kutulinda tusigharamike zaidi,” akasema mmoja wa maafisa wa mashirika hayo.

Kulingana na CMA, kampuni nne kubwa za utengenezaji unga -Mombasa Millers, Pembe, Kitui Millers na Dola- ndizo zenye akiba ya mahindi, japo hayatoshi kukimu mahitaji ya soko kwa wiki tatu zijazo, ikiwa hayataongezwa.

NCPB ilinunua magunia 417,000 ya kilo 90 za mahindi kwa Sh2,300 msimu huu, kinyume na magunia milioni mbili, yaliyokuwa yametarajiwa.

“Tuna magunia milioni 3.5 ya mahindi ya msimu uliopita na 417,000 ambayo tulinunua msimu huu,” Bw Maiyo akasema awali.