Makala

Hofu mauaji katika shamba la Del Monte huenda yaibue uasi kama wa Mau Mau

January 2nd, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

Uhasama kati ya walinzi wa shamba la Kimarekani la ukuzaji mananasi ya Del Monte na majirani wake ambao huzua mashambulizi ya mauti umesemwa kuwa hatari na unaoweza kuzua hisia za Vita vya Mau Mau.

Aidha, ni suala ambalo hata limezuwa mgawanyiko kati ya wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa mirengo miwili, mmoja ukisema haujivunii kuhusishwa na ukatili wa mauaji na wengine wakishabikia hali hiyo ya majonzi.

Hii ni baada ya visa vya mauaji dhidi ya vijana wa kiume ambao hudaiwa kuvamia shamba hilo kwa nia ya kuiba mananasi hayo kuongezeka kwa kiwango kikuu, katika kipindi cha wiki mbili sasa kukiripotiwa mauaji ya vijana wanane.

Kisa cha hivi karibuni ni cha Desemba 24, 2023 ambapo vijana wanne walipatikana katika Mto Chania wakiwa na majeraha ya kupigwa, kupondwa, kukatakatwa na kunyongwa, wote wakiwa ni wa kutoka Kaunti ya Machakos.

Katika vituo vya polisi vya Makongeni, Thika na Ngati huwa kila siku kunafikishwa vijana ambao wamekamatwa wakiwa na hata majeraha ya kuraruliwa na majibwa ya walinzi hao huku wenyeji sasa wakisema serikali husaidia kampuni hiyo kuvumisha dhuluma dhidi ya binadamu.

Licha ya kuwa kampuni hiyo kupitia taarifa kadha za mkurugenzi wake mkuu Bw Stergios Gkaliamoutsas zikiahidi kuchunguza visa hivyo ambavyo hata vimefanya baadhi ya masoko duniani kuweka masharti dhidi ya bidhaa za Del Monte, mauti hayo na majeraha yamekuwa yakizidi kuchipuka kila kuchao.

Shamba hilo ambalo liko katika Kaunti ya Murang’a la zaidi ya ekari 28, 000 limepakana na Kaunti za Machakos na Kiambu na hutoa ajira ya moja kwa moja kwa zaidi ya watu 6,500 huku wengine 28, 000 wakilitegemea kutokana na ugatuzi wa manufaa.

Baada ya kisa hicho cha miili minne kutolewa kutoka mto na kuzua kilio, mahangaiko, hasira na maombi ya laana kutoka kwa wapendwa wao, wanasiasa na watetezi wa haki za kibinadamu, mjadala ulitanda ndani ya wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Huku wengine wakiungana na Seneta wa Murang’a Joe Nyutu, mwenyekiti wa Muungano wa Wakazi wa Kandara Bw Kibiru Mwangi kukemea washukiwa wa mauaji hayo na ambao ni walinzi wa kampuni hiyo, wengine walishikilia kuwa maafa hayo huzuka katika mazingara ya kivita wala sio dhuluma.

Katika mitandao yao ya kijamii, baadhi ya wafanyakazi hao walishikilia kauli ya rais William Ruto kwamba wakora “aidha wakome, wahame au wasafirishwe hadi mbinguni”.

Nao wengine waliteta kwamba liwe liwalo, uhai wa binadamu ni wa kuheshimiwa na unafaa tu kutwaliwa na aliyeutoa akiwa ni Mungu muumba yote.

Wengine walipinga wakisema kwamba ni sharti watu waheshimu mali ya wenyewe nao wengine wakijibu kwamba walinzi hawakuua bali walisafirisha wakisafisha ukora katika jamii.

Katika ile hali ya ujeuri na ujanja, kunao walihoji kama kunaye aliye na ushahidi kwamba wanne hao na wengine wengi kwa kweli huuawa na walinzi hao?

“Huenda hao vijana waliuawa na wakubwa wa kwao ambao wanasema kuna genge la Mungiki linalojiunda…licha ya kuwa kampuni yetu inajipa sifa mbaya, hao watu pia wanakubali hadharani kuwa vijana wao huiba mananasi katika shamba la Del Monte,” akasema mwingine.

Mfanyakazi mwingine aliwaelezea wenzake kwamba “kabla muamze kuhukumu walinzi wetu, mnafaa muelewe kwamba kunao ambao wamepata majeraha mabaya wakilinda kazi zao na pia kampuni yetu dhidi ya wavamizi hao”.

Aliteta kuwa waandishi wa habari, viongozi wengine na pia wanasiasa huwaponda walinzi hao “bila kwanza kuzingatia kwamba kuna mifano tele ya hatari ya kazi”.

Kwa mfano, akatoa, “kunaye hata aligeuzwa kuwa wazimu alipogongwa na mawe kichwani, mwingine hana jicho moja huku hata kukiwa nao ambao pia wameaga dunia mikononi mwa wavamizi hao”.

Baadhi ya wafanyakazi hao waliteta kwamba “kampuni hii yetu inafaa itafute mbinu mbadala ya kukabiliana na wezi wa mananasi kwa kuwa hakuna manufaa ya kuhusishwa na mazingara ya mauaji”.

Wafanyakazi wengi waliitaka kampuni hiyo yao kuweka ua ili kuwatatiza wezi na pia kuongeza idadi ya walinzi.

“Aidha, kuna walinzi wengine ambao hushirikiana na wavamizi hao kupitia kuwauzia mananasi na hali hugeuka ya vita wakati wale ambao sio wafisadi wameamua kuwakabili wezi hao,” akasema mwingine.

Hayo yakijiri, Bw Nyutu alisema kwamba “ni lazima kampuni ya Del Monte ijizatiti kuheshimu haki za kibinadamu kwa kuwa hakuna aliye na ruhusa ya kuchukua sheria mkononi hasa kutekeleza mauaji”.

Bw Nyutu alisema hatachoka kukumbusha Del Monte kwamba “ninyi mko hapa mkitumia rasilimali za Wakenya na ambao ndio wenye nchi na mamlaka yake na juu yenu kutafuta njia za kisheria za kuhakikisha mananasi yenu yako salama na wavamizi wanakabiliwa kwa mujibu wa sheria”.

Mwanasiasa huyo wa Murang’a alisema kwamba “hamuwezi kukuza mananasi kandokando mwa barabara za umma pasipo na ua lolote halafu mjidanganye kwamba hamutalengwa na wezi wa mavuno yenu”.

[email protected]