Hofu Mlimani kuhusu unaibu rais

Hofu Mlimani kuhusu unaibu rais

NA BENSON MATHEKA

WASIWASI umetanda katika eneo la Mlima Kenya kwamba huenda likakosa wadhifa wa naibu rais kwenye serikali ijayo huku washirika wa wagombeaji wakuu kutoka maeneo mengine wakishinikiza wateuliwa wagombea wenza.

Hofu hii imeongezeka baada ya kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kujiunga na muungano wa Azimio La Umoja ambalo limemuidhinisha kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuwa mgombea urais wake.

Katika muungano wa Kenya Kwanza ambao mgombea urais wake ni Naibu Rais William Ruto, chama cha Amani National Congress (ANC) kinashinikiza kiongozi wao, Musalia Mudavadi ateuliwe mgombea mwenza.

Shinikizo hizi, zimezua hali ya wasiwasi miongoni mwa wanasiasa na wapigakura katika eneo la Mlima Kenya waliotarajia kuwa miungano hiyo miwili mikuu ililitengea wadhifa wa naibu rais moja kwa moja kwa kuwa lina kura zaidi ya milioni sita na halina mgombea urais maarufu.

Ingawa wadhifa ambao Bw Musyoka aliahidiwa Azimio La Umoja likishinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9 haujabainika, duru zinasema kwamba mojawapo ya masharti yake ya kujiunga na muungano huo unaojumuisha Rais Uhuru Kenyatta, ni kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.

Inasemekana viongozi wa chama cha Jubilee kutoka Mlima Kenya waliokuwa wakimezea mate wadhifa huo wanahofia kwamba huenda ukamwendea Bw Musyoka.

“Wasiwasi wetu ni kuwa huenda eneo letu likakosa kuwakilishwa kikamilifu katika serikali ijayo iwapo Bw Odinga atashinda urais akiteua Musyoka kuwa mgombea mwenza wake. Tumewekeza nguvu, muda na rasilmali zetu kuvumisha Azimio La Umoja kwa matumaini kwamba eneo letu litanufaika na wadhifa wa naibu rais katika serikali ya Bw Odinga na kuna dalili huenda hilo halitatimia,” akasema mbunge mmoja wa chama cha Jubilee kutoka kaunti ya Nyeri ambaye aliomba tusitaje jina.

Baadhi ya waliopigiwa upatu kwa wadhifa wa mgombea mwenza wa Bw Odinga ni aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth, Waziri wa Kilimo Peter Munya, Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi, mwenzake wa Nakuru Lee Kinyanjui na kiongozi wa chama cha Narc-Kenya Martha Karua.

Kenneth, Muriithi na Kinyanjui wamekuwa wakimpigia debe Bw Odinga na kuvumisha Azimio La Umoja eneo la Mlima Kenya.

Bi Karua ni mmoja wa vinara wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) ambao kulingana na Bw Musyoka, utakuwa mshirika katika Azimio La Umoja.

Bw Muriithi na Bw Kinyanjui wanatatea viti vyao vya ugavana kupitia vyama tanzu vya Azimio La Umoja.

Bw Munya alitupilia mbali azma yake ya kugombea kiti cha ugavana kaunti ya Meru baada ya kuahidiwa wadhifa katika serikali ya Azimio La Umoja.

Japo Dkt Ruto amekuwa akiahidi wakazi wa Mlima Kenya kwamba litawakilishwa kwenye serikali yake akishinda urais, wasiwasi umeibuka baada ya wanasiasa wa ANC kumshinikiza ateue Bw Mudavadi kwa wadhifa huo.

Kulingana na seneta wa Kakamega Cleopas Malala, ANC ni mshirika wa United Democratic Alliance (UDA) cha Dkt Ruto katika muungano wa Kenya Kwanza Alliance unaojumuisha Ford Kenya kinachoongozwa na Moses Wetangula na wadhifa huo unafaa kuwa wao.

“Wakati huu, tunatoa sharti kwamba huu ni muungano wa vyama, sio muungano wa maeneo. Watu hawawezi kusema kwamba kwa kuwa wanatoka eneo la Mlima, wanafaa kuwa naibu rais na sio sisi. Sisi kama chama tunasema UDA ikichukua urais, basi ANC inafaa kuchukua wadhifa wa naibu rais,” akasema Bw Malala.

Miongoni mwa washirika wa Ruto kutoka Mlima Kenya waliopigiwa upatu kuwa wagombea wenza wake ni mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, mwenzake wa Kandara, Alice Wahome, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na seneta wa Tharaka Nithi Profesa Kithure Kindiki.

Duru zinasema takwa la Bw Malala limezua mchecheto miongoni mwa washirika wa Dkt Ruto Mlima Kenya ambao wamemuunga mkono kwa miaka minnne wakiuza sera zake kabla ya kuungana na Bw Mudavadi na Bw Wetangula yapata miezi miwili iliyopita.

You can share this post!

Lenku apigwa jeki wazee wa Agikuyu wakiunga azma ya kutetea...

TUSIJE TUKASAHAU: Wito wa Rais Kenyatta kaunti zilipe...

T L