Hofu Mswada kusukuma raia kwa bidhaa ghushi

Hofu Mswada kusukuma raia kwa bidhaa ghushi

NA BENSON MATHEKA

WAKENYA wengi watageukia bidhaa haramu iwapo Mswada wa Fedha 2022 utapitishwa na Bunge la Kitaifa, utafiti uliofanywa na shirika la Stop Crime Kenya ( StoCK), unaonyesha.

Utafiti huo unasema kwamba kupitishwa kwa mswada huo unaolenga kuongeza ushuru wa bidhaa muhimu ikiwemo unga wa mahindi, kutawafanya Wakenya maskini washindwe kumudu bei za bidhaa hizo.

Wabunge wanajadili mswada ambao unapendekeza kuongezwa kwa ushuru wa bidhaa hizi katika juhudi za serikali kufadhili bajeti ya Sh3.3 trilioni.

Ukipitishwa

Ukipitishwa kuwa sheria, bei za bidhaa kama unga, juisi, maji ya chupa, pombe, mvinyo na sigara zitaongezeka.

“Kuongezeka kwa bei hizi, pamoja na mfumko wa gharama ya maisha, kutalemea Wakenya wakati ambao wengi wanang’ang’ana kukabiliana na kupanda kwa gharama ya maisha sawa na watengenezaji bidhaa ambao wanakabiliwa na gharama ya juu ya uzalishaji,” unasema utafiti huo.

Mwenyekiti wa StoCK, Bw Stephen Mutoro, alieleza kwamba raia wengi wanatarajiwa kutafuta bidhaa za bei nafuu na duni ambazo ni vigumu kuthibiti kwa kuwa zinauzwa kwa njia ya magendo hatua ambayo itachochea biashara haramu na kunyima serikali mapato.

Utafiti Kulingana na utafiti huo, Wakenya wawili kati ya watatu wanaamini kwamba Mswada huo ni juhudi za serikali za kuziba pengo la Sh153 bilioni linalosababishwa na biashara ya magendo ambayo imeshindwa kuizima.

Aidha, utafiti unafichua kuwa kupitishwa kwa mswada huo huenda kukaathiri matokeo ya uchaguzi mkuu ujao.

Watu wanne kati ya watano waliohojiwa walisema kwamba kupanda kwa bei za bidhaa muhimu kutawafanya wabadilishe uamuzi wao kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Utafiti ulibaini kwamba tayari asilimia 20.8 ya Wakenya wanasema kwamba tayari wanatumia bidhaa haramu kwa kuwa ni nafuu, huku asilimia 55 wakisema kupanda kwa ushuru kutawafanya wageukie bidhaa hizo.

Kwa kawaida, bidhaa za magendo huwa hazitozwi ushuru na kuongezeka kwa biashara hiyo kutanyima serikali mapato.

Wakenya wawili kati ya watatu walioshirikishwa kwenye utafiti, wanaamini kwamba watumiaji bidhaa watatumiwa kufidia kushindwa kwa serikali kuzuia wahalifu wanaoendesha biashara haramu nchini, ambao inasemekana wanakwepa kulipa ushuru wa ShSh419 milioni kila siku.

Jukumu la serikali

Bw Mutoro alieleza kuwa kulingana na utafiti, asilimia 45 ya Wakenya, wanaamini kwamba serikali inapaswa kutumia pesa zaidi kukabili biashara haramu japo asilimia 21.7 wanaamini kwamba hata ikifanya hivyo haitapata ushuru zaidi.

“Utafiti wetu huu wa hivi punde unaonyesha kwa mara nyingine ukosefu wa uhalisia kati ya watungaji sera na hali halisi ya maisha ya watumiaji bidhaa wa kawaida ambao wanang’ang’ana kukabiliana na kupanda kwa gharama ya maisha,” alisema Bw Mutoro.

Anasema kwamba kuongezwa kwa ushuru kunatisha kusukuma Wakenya wanaotia bidhaa kufanya kazi halali kuingia katika sekta ya biashara haramu kupata bidhaa nafuu.

“Kwa kufanya hivyo, raia wanawekwa kwenye hatari ya kutumia bidhaa duni ambazo hazithibitiwi huku wahalifu wakitajirika na Hazina ya Taifa kunyimwa mapato inayohitaji,” asema.

  • Tags

You can share this post!

Wahubiri 400 wapokea mafunzo maalum

Barcelona wakamilisha La Liga msimu huu kwa alama chache...

T L