Habari

Hofu Mungiki wakirejea kuhangaisha wakazi

October 22nd, 2018 2 min read

NICHOLAS KOMU na JOSEPH WANGUI

WASIWASI umetanda kwamba kundi la Mungiki limeibuka upya na sasa linasajili hata watoto wa shule katika eneo la Kati.

Maafisa wa usalama tayari wamewakamata watu zaidi ya 90 kwa kuhusishwa na kundi hilo linalofahamika kwa ukatili dhidi ya raia.

Kwa kawaida kundi hilo hutoweka kwa muda kisha kurejea kwa mfumo mpya na jina jipya.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibainisha kwamba wakati huu genge hilo linajificha chini ya kikundi cha wahalifu cha Gaza kilicho mtaa wa Kayole, Kaunti ya Nairobi.

Wanachama wa kikundi hicho hutambuliwa kwa mavazi yao ya jeans zinazobana, viatu aina ya ndara, na kofia za aina ya kipekee ambazo sasa zinavaliwa na wanachama wa Mungiki.

Kikundi hicho pia hufahamika kwa mavazi yao ya shati zinazofanana na za skauti au za kijeshi.

Wamekita kambi katika maeneo ya Mwea na Kutus yaliyo Kaunti ya Kirinyaga, Nyeri Mjini na Kiriaini katika Kaunti ya Murang’a na sehemu za Kaunti ya Nyandarua.

Hata hivyo, inaaminika ngome yao kuu ni katika mtaa wa mabanda wa Kiandutu na Makongeni katika eneo la Thika.

Sawa na jinsi ilivyokuwa zamani, wanachama wa kikundi hicho hutoza ada kutoka kwa wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma katika mitaa mbalimbali wakidai ni ada za kupeana usalama kwa biashara hizo.

Wamekuwa pia wakiitisha malipo kutoka kwa sehemu za ujenzi na biashara nyingine mbalimbali.

Wapelelezi walisema kikundi hicho kinajijenga kifedha kwa kutoza pesa kwa njia za utapeli kutoka kwa wananchi na pia kwa kuibia raia.

Ingawa hawajaonekana kutumia ukatili na mauaji kama ilivyokuwa zamani, wananchi ambao wanafahamu kuhusu uwepo wao wanahofia kuzungumza kuwahusu.

Wale ambao walikubali kuhojiwa waliomba wasitajwe majina.

Mzazi aliyeomba asitajwe kwa kuhofia kikundi hicho alifichua kwamba kuna wavulana walio wanafunzi wa shule za upili ambao wanasajiliwa kujiunga na Mungiki.

“Wamekuwa watundu sana na baada ya kusukumwa kufichua kilichobadili tabia zao, walikiri kwamba walisajiliwa kujiunga na kikundi kinachotambulika kama Gaza. Wao huibia watu kwa niaba ya kikundi hicho kisha wanalipwa asilimia ya kiwango wanachopeleka. Wazazi wengi wanahofia hata kupiga ripoti kwa polisi kwa sababu hatujui hiki kikundi kina ushawishi wa kiwango gani,” akasema.

Wahudumu wa boda boda pia wamekuwa waathiriwa wa kikundi hicho kinachowatoza ada, na wanashuku kuna baadhi yao ambao hushirikiana na genge hilo.

Imefichuka kwamba wakati Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, alipokutana na wakuu wa usalama Nyeri hivi majuzi, aliagiza msako uanzishwe dhidi ya kikundi hicho na kivunjiliwe mbali kabla siku 100 zikamilike.