Hofu njaa kuleta vurugu za kijamii

Hofu njaa kuleta vurugu za kijamii

NA WAANDISHI WETU

HOFU ya mashambulizi kati ya jamii za wafugaji na wakulima imeanza kuibuka, huku zaidi ya watu 500,000 wakiripotiwa kukumbwa na baa la njaa katika ukanda wa Pwani.

Kulingana na shirika la Kenya Red Cross, Kaunti za Tana River, Kilifi, Kwale, Lamu na sehemu za Taita Taveta ndizo zilizoathirika Pwani.

Afisa mkuu wa shirika hilo Pwani, Bw Hassan Musa, alisema pia mizozo kati ya binadamu na wanyamapori inahofiwa kuongezeka, wanyama wanapotoka mwituni kutafuta lishe na maji vijijini.

“Wanaoathirika zaidi na baa la njaa ni kina mama wanaonyonyesha na watoto chini ya umri wa miaka mitano ambao wamepatikana na maradhi ya utapiamlo,” akasema Bw Musa.

Athari za kiangazi zinatarajiwa kuongezeka kwani mashirika ya kutabiri hali ya hewa nchini na kimataifa yalibashiri hakutakuwa na mvua ya kutosha msimu wa mvua kuanzia mwezi huu hadi Desemba.

Hata hivyo, Bw Musa aliwahakikishia waathiriwa wa janga la njaa kuwa kuna mipango inayoendelezwa kuwasaidia.

“Kupitia juhudi za mashirika tumesaidia familia 80,000 eneo la Pwani. Katika Kaunti ya Tana River, familia 1,300 zimepokea Sh5,400 kwa kipindi cha miezi miwili ili wajikimu,” akasema Bw Musa.

Alisema pia wanawahamasisha wafugaji dhidi ya kuacha mifugo yao ivamie mashamba ya wakulima.Gavana wa Kaunti ya Tana River, Bw Dhadho Godhana, alisema kwa sasa kaunti haina pesa za kusaidia waathiriwa wa njaa.

Alisema pesa zilizotengewa misaada ya dharura ziliisha katika mwaka wa kifedha uliopita na sasa wanategemea tu misaada kutoka kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Ukame (NDMA).

“NDMA kwa sasa ina pesa kwa hivyo sisi tunasaidia tu kwa kuwapa malori ya usambazaji,” akasema.

Bw Godhana pia alilaumu serikali ya kitaifa kwa kutojumuisha kaunti hiyo miongoni mwa zilizohitaji kusambaziwa vyakula vya misaada.

Diwani wa Wadi ya Hirimani, Bw Ishmael Kodobo, alisema eneobunge la Bura limeathirika zaidi.Kulingana na NDMA, zaidi ya watoto 22,000 katika kaunti hiyo wanakumbwa na utapiamlo.

“Bura imeathirika zaidi ikifuatwa na Galole. Hakuna kidimbwi chochote wala bwawa lililo na maji. Wakazi wanatembea zaidi ya kilomita 25 kutafuta maji,” akasema mratibu wa NDMA katika kaunti hiyo, Bw Abdi Musa.

Mbunge wa Ganze, Kaunti ya Kilifi, Bw Kenneth Kazungu, alisema atawekeza kwenye kilimo cha kunyunyuza maji katika eneobunge lake kama suluhu ya kudumu kwa kuzalisha chakula bila kutegemea mvua.

Bw Kazungu aliongeza kuwa serikali ya kitaifa inapaswa kuchimba mabwawa ya kutosha ya kuhifadhi maji.

“Miaka 60 tangu Kenya kupata uhuru wake eneobunge langu bado linategemea chakula cha msaada. Wakazi wa Ganze hulima sana wakati wa mvua lakini changamoto imetokana na mabadiliko ya hali ya anga. Ni miaka mitatu sasa na hatujaona mvua,” akasema.

Katika Kaunti ya Lamu, wakazi katika kijiji cha Ishakani mpakani mwa Lamu na Somalia na wengine wa kijiji cha Pandanguo, wanahitaji msaada wa dharura.

Mzee wa Nyumba Kumi kwenye kijiji cha Ishakani, Bw Ahmed Islam, alisema maji ya mvua waliyokuwa wamehifadhi yameisha.

Alisema mara nyingi walikuwa wakitegemea maafisa wa jeshi kuwasambazia maji kupitia kwa malori yao wanapokuwa na mahitaji lakini wakati huu hawajasaidiwa.

Kwa upande wake, msemaji wa jamii ya Waboni kijijini Pandanguo, Bw Ali Sharuti, alisema wananchi wanalazimika kulala bila kula wala kuoga kwani visima, vidimbwi na mito waliyotegemea kuchota maji imekauka kutokana na kiangazi.

Bw Sharuti alisema mimea waliyokuwa wamepanda yote ilinyauka kufuatia ukame uliokithiri.

Kwenye kijiji cha Ishakani, wakazi hutegemea maji wanayovuna kutoka kwa mvua na kuyahifadhi kwenye matangi maalum kwa matumizi yao ya kila siku.

Kijijini Pandanguo, wakazi hutegemea visima, mito na vidimbwi kupata maji yao ya matumizi ya nyumbani.

  • Tags

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Viongozi wa eneo la Nyanza...

Njama ya Kenya Kwanza kuzika ODM Pwani

T L