Kimataifa

Hofu tele China virusi hatari vikiua karibia watu 10

January 22nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MTU wa tisa amefariki China kutokana na aina mpya ya virusi ambavyo vimesambaa kwa kasi kote nchini humo, huku mamlaka ikithibitisha kwamba vinaweza kuenezwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

Virusi hivyo vinafanana na vile vya SARS

Naibu mkurugenzi wa Tume ya Afya nchini China, Li Bin, amethibitisha kwenye kikao cha Jumatano jijini Beijing.

Mwanamume aliyekuwa na umri wa miaka 89 kutoka mji wa Wuhan ambao ndio kitovu cha mkurupuko huo alikuwa mhanga wa hivi majuzi wa aina mpya ya virusi hivyo vya mapafu vinavyosababisha aina fulani ya nimonia.

Visa vya maambukizi zaidi ya 440 sasa vimeripotiwa katika miji mikuu nchini China ikiwemo Beijing na Shanghai.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linatathmini kuhusu kutangaza dharura ya afya ya umma kimataifa kuhusiana na virusi hivyo; jinsi ilivyofanya na homa ya nguruwe na Ebola.

Uamuzi utafanywa katika mkutano hii leo Jumatano.

Tume ya Afya Nchini China mnamo Jumatatu ilithibitisha kwa mara ya kwanza kwamba ugonjwa huo unaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

Ilisema watu wawili katika mkoa wa Guangdong walikuwa wameambukizwa kwa njia hiyo.

Katika taarifa tofauti, Tume ya Afya katika Manispaa ya Wuhan ilisema kuwa maafisa wa afya wapatao 15 mjini Wuhan pia wameambukizwa virusi hivyo, huku mmoja wao akiwa katika hali mahututi.

Wafanyakazi hao yamkini waliambukizwa virusi hivyo kutokana na kutangamana na wagonjwa hao.

Matabibu hao wote wamewekwa katika sehemu zilizotengwa huku wakitibiwa.

Ugonjwa huo uligunduliwa kwa mara ya kwanza mjini Wuhan, eneo la kati, Uchina, lenye watu milioni 11, mwishoni mwa mwaka uliopita.

Kwa sasa kuna visa 218 vilivyothibitishwa vya virusi hivyo Uchina kulingana na WHO.

Visa kadha pia vimethibitishwa kwingineko: viwili Thailand, kimoja Japan, na kingine Korea Kusini ambapo walioambukizwa walikuwa wamerejea majuzi kutoka Wuhan.

Rais wa China Xi Jinping ametoa wito kwa “juhudi za kila namna” za kudhibiti mkurupuko huo kulingana na vyombo vya habari nchini humo, ikiwemo “kutoa habari na kuchukua hatua za kuelekeza maoni ya umma.”

Mamlaka katika mataifa mengi ikiwemo Australia, Singapore, Hong Kong, na Japan zimezidisha uchunguzi wa abiria wa ndege kutoka Wuhan.

Mamlaka ya Amerika wiki iliyopita ilitangaza hatua sawa na hizo katika viwanja vya ndege vya San Francisco, Los Angeles na New York.

Virusi hivyo vinavyofahamika pia kama 2019-nCoV, vinaeleweka kuwa aina mpya ya virusi vya mapafu ambavyo havijawahi kutambuliwa hapo mbeleni katika binadamu.