Habari Mseto

Hofu vifo kutokana na Covid-19 vikiendelea kuthibitishwa

November 20th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KENYA Alhamisi iliendelea kuandikisha idadi kubwa ya watu wanaofariki kutokana na Covid-19 baada ya wagonjwa 17 zaidi kuthibitishwa kufariki kutokana na ugonjwa huo hatari.

Idadi jumla ya waliofariki imefika 1, 330.

Kwenye taarifa iliyotumiwa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kwa vyombo vya habari, watu wengine 1,459 walithibitishwa kuambukizwa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa huo ndani ya saa 24 zilizopita.

Visa hivyo vipya vimefikisha idadi jumla ya maambukizi ya corona nchini kuwa 74,145 tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa huo kilipogunduliwa nchini mnamo Machi 13, 2020.

Wagonjwa hao wapya walipatikana baada ya sampuni kutoka watu 10,146 kupimwa; hatua ambayo imefikishwa idadi jumla ya vipimo kuwa 815,040 tangu Machi mwaka huu.

Visa hivyo vipya vimesambaa nchini kama ifuatavyo huku kaunti ya Nairobi ikiongoza kwa visa 472, ikifuatwa na Kiambu yenye visa 311,

Kaunti ya Mombasa inashikilia nambari tatu kwa kuandikisha visa 108, Laikipia (63), Uasin Gishu (53), Busia (49) , Kisumu (48) , Meru (43) , Nakuru (36), Kericho (33), Kisi (29), Kakamega (29), Marsabit (17), Murang’a (16), Nyamira (16), Kajiado (15), Garissa (13), Nandi (12), Kitui (12), Nyeri (11) na Machakos visa 11.

Vile vile, Siaya ina visa vipya (10), Bungoma (10), Turkana (8), Kirinyaga 8, Kilifi (6), Bomet (5), Trans Nzoia (4), Homabay (3), Makueni Taita Taveta na Kwale vikiwa na visa viwili kila moja huku Isiolo na Tharaka Nithi zikiandikisha kisa kimoja kila moja.

Waziri Kagwe aliongeza kuwa kuna wagonjwa 1,116 ambao wamelazwa katika hospitali mbali mbali nchini ilhali wengine 6,232 wanauguzwa nyumbani.

“Wagonjwa wengine 59 wamealazwa katika Vyumba vya kuwahudumia Wagonjwa Mahututi (ICU), 27 wanasaidiwa kupumua kwa kutumia vifaa maalum ilhali wengine 28 wanaongewa hewa ya Oksijeni,” taarifa hiyo ikasema.

Wakati huo huo, wagonjwa 780 wamethibitishwa kupona Covid-19 ambapo 690 walikuwa chini ya mpango wa utunzaji nyumbani ilhali 90 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali. Idadi jumla ya waliopona sasa imegonga 50,658 kufikia Alhamisi, Novemba 19, 2020.