HabariSiasa

Hofu wabunge 17 wana virusi vya corona

April 8th, 2020 2 min read

 SAMWEL OWINO na FATUMA BUGU

KIKAO maalum cha wabunge kimeahirishwa kwa muda usiojulikana kutokana na hofu kuwa baadhi ya wabunge wameambukizwa virusi vya corona.

Duru za kuaminika kutoka bunge zimearifu Taifa Leo Dijitali kuwa ingelikuwa hatari kwa wabunge kuendeleza kikao kilichopangwa kufanyika siku ya Jumanne kabla ya kutolewa kwa majibu ya wanachama 50 waliofanyiwa vipimo vya virusi vya corona.

Taarifa kutoka kwa maafisa mbalimbali ndani ya bunge zilionyesha kuwa angalau wabunge 17 kati ya 50 waliofanyiwa uchunguzi wameptikana na ugonjwa wa corona.

Hata hivyo, spika wa bunge, Justin Muturi alipinga madai hayo na kudai ni habari za uongo.

“Sio ukweli,” Bw Muturi alisema. “Majibu ya vipimo yalitolewa kwa wahusika pekee.”

Pia, Michael Sialai, karani wa bunge, alisema hatambui kuwepo kwa visa 17 vya corona .

“Hapana, sina ripoti hiyo. Vipimo vilifanywa na matokeo yalikabidhiwa watu binafsi,” alisema Bw Sialai.

Kiongozi wa Wengi bungeni, Adan Duale alikataa katakata kuwepo kwa ripoti hiyo. “Sifahamu lolote kuhusiana na jambo hilo, nadhani ni porojo tu,” alisema Bw Duale.

Visa hivyo 17 vya maambukizi ya corona havikutajwa katika maelezo ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe siku ya Jumanne, ambapo alitaja kuwepo kwa visa 14 tu vya maambukizi mapya ya corona.

Kulingana na jumbe fupi kupitia simu zilizotumwa na karani wa bunge siku ya Jumatatu, kikao hicho kiliahirishwa kutokana na mikakati ya kupanga njia madhubuti za kuhakikisha usalama wa wabunge na wafanyikazi katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Kiongozi wa Wachache, John Mbadi ambaye ni mmoja wa waliofanyiwa vipimo vya virusi vya corona, alisema kuwa bado angali anasubiri majibu yake na kuhakikisha kuwa wizara ilionya kuendelezwa kwa vikao bila uwepo wao.

“Tusiwahukumu waathiriwa wa ugonjwa wa corona, kama mtu ni mgonjwa….ni hali tu na anaweza kupona,” alisema Bw Mbadi. “Tunapaswa kuwahimiza kujitokeza na kufanyiwa vipimo hivyo,” aliongeza Bw Mbadi.

Aidha, kulingana na ripoti za kuaminika, huenda wabunge na wafanyikazi zaidi ya 50 walijumuika na mbuge wa Rabai, Bw Kamoti Mwanamkale, ambaye alipatikana na virusi vya corona na hivyo, vikao vya bunge vikahatarisha maisha ya wanachama wengine kwa kuruhusu vikao kufanyika.