Habari Mseto

Hofu wafungwa 118 wakiambukizwa corona Bungoma

October 12th, 2020 1 min read

Na BRIAN OJAMAA

HALI ya wasiwasi imezuka katika Gereza la Bungoma baada ya wafungwa 118 kuthibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.

Afisa Mkuu wa Afya katika kaunti hiyo, Patrick Wandili, alithibitisha tukio hilo, akisema kuwa kuna uwezekano wafungwa zaidi wemeambukizwa.

Alisema kuwa virusi hivyo vipo, hivyo wakazi wanapaswa kuzingatia masharti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kudhibiti maambukizi yake.

“Tunawarai wananchi kuzingatia kanuni za kutokaribiana, wavae barakoa na kuosha mikono yao kila mara kwani virusi hivi ni hatari,” akasema.

Afisa mmoja ambaye hakutaka kutajwa alisema kuna uwezekano virusi hivyo vilisambazwa na wafungwa wanane ambao walithibitishwa kuambukizwa corona mwezi uliopita.

Wafungwa hao walipelekea katika kituo cha afya cha Webuye, ambako kuna karantini inayosimamiwa na kaunti.

Hata hivyo, wafungwa hao walirejeshwa gerezani baada ya mmoja wao kutoroka kutoka karantini usiku katika hali tatanishi.

Afisa huyo alisema kwamba gereza hilo lina msongamano mkubwa, hali ambayo huenda ilichangia wafungwa wengi kuambukizana.

Sampuli za wafungwa zaidi na maafisa waliotangamana nao zimepelekwa katika Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu Kenya (KEMRI) jijini Kisumu ili kupimwa.

Wiki iliyopita, Seneta Moses Wetang’ula wa Bungoma alimlaumu Gavana Wycliffe Wangamati kwa kutotumia vyema Sh213 milioni ambazo kaunti ilipewa na Serikali ya Kitaifa kukabili janga hilo.

Hata hivyo, Bw Wangamati alikanusha madai hayo, akisema wametumia robo tu ya fedha hizo.