Habari Mseto

Hofu wanaume 3 kuhudhuria misa wakiwa wamebeba shoka

November 11th, 2019 1 min read

 NA FRANCIS MUREITHI

WAUMINI wa Kanisa Katoliki la St Joseph katika mtaa wa Race-track Jumapili waliingiwa na kiwewe baada ya wanaume watatu waliojihami kwa shoka kufika kwenye misa wakiwa wamejihami kwa shoka.

Watatu hao waliingia kanisani saa 12.45 asubuhi wakati Padri Evans Njogu ambaye alikuwa amerejea kutoka likizo ya miezi mitano nchini Marekani alikuwa akiongoza misa ya kwanza.

Hata hivyo, hakuwa na habari kwamba wanaume hao watatu hatari walikuwa miongoni mwa waumini wake.

Kulingana na waumini wengine, watatu hao walikuwa wamevaa rosari na mashemasi walianza kushuku nia yao kwa kuwa walikuwa wakiondoka nje na kurudi ndani kila mara.

“Tuliwapasha habari chama cha wanaume wanaoshiriki kanisani ambao waliungana na kuweka ulinzi mkali langoni na maeneo mengine ya kuingia ndani. Hata hivyo, walikamatwa misa ilipokamilika na wakapatikana wakiwa wamejihami kwa shoka,” akasema muumini moja.

Kinaya ni kwamba kanisa hilo lina walinzi langoni ila muumini mwengine alilalamika kwamba hawakumakiniki kazi yao kama Jumapili iliyopita.

“Walikuwa wakipiga gumzo na wakakosa kuwajibika jinsi wao hufanya kila Jumapili. Nilipita langoni bila kupekuliwa,” akasema

“Kuna shida sana katika kuhakikishia waumini usalama wao kama watu wanaweza kuingia kanisani wakiwa wamejihami kwa silah hatari,” akasema mwengine.