Hofu wasichana wateswa chuoni na ‘masponsa’

Hofu wasichana wateswa chuoni na ‘masponsa’

NA MAUREEN ONGALA

USIMAMIZI wa Chuo Kikuu cha Pwani, umeeleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la wanafunzi wa kike wanaopitia dhuluma mikononi mwa wanaume wanaowasaidia kujikimu, almaarufu ‘masponsa’.

Msimamizi wa masuala ya jinsia katika chuo hicho, Bi Riziki Yusuf, ameeleza kuwa, wanafunzi hao hupigwa na wapenzi wao ambao baadhi yao wanaishi nao.

Akizungumza na Taifa Leo, Bi Yusuf alisema licha ya kuwa wanafunzi hao wa kike hupigwa na kuumizwa, hawataki kuachana na uhusiano huo na wengi wao huamua kuvumilia kwa sababu ya umaskini.

“Wengi hata baada ya kupiga ripoti kwangu hawataki kuchukua hatua za kisheria kwa wahusika kwa sababu ndio tegemeo lao,” akasema.

Hali hiyo inasemekana kuwafanya baadhi ya waathiriwa kupitia matatizo ya akili.

Alifafanua kwamba wengi wa wanafunzi wanaodhulumiwa ni maskini na hulazimika kung’ang’ana na maisha wakiwa chuoni.

Wanapojiunga na chuo katika mwaka wa kwanza huwa wamefanyiwa michango ya kuwawezesha kujikimu, lakini wanapoingia muhula wa pili, hali huwa ngumu kwani wazazi wao hukosa kuwashughulikia.

Hapo ndipo wengi wao hujihusisha na mapenzi ovyo ili waendelee na masomo yao.

Umaskini

“Inasikitisha kuwa kuna baadhi ya wanafunzi ambao waliamua kuacha shule kwa sababu ya umaskini na kwa sasa wanaendeleza biashara ya ngono mjini Kilifi,” akasema.

Bi Yusuf alisema baadhi ya wanaume wanaotegemewa ni wanafunzi wenza ambao wana uwezo wa kifedha.

“Imekuwa vigumu kwetu kuwaondoa wasichana hawa katika mahusiano hayo ambayo yamejaa dhuluma za jinsia na kila mara tunapojaribu kuwatengenasha tunagundua kuwa wamerudiana na bado wanadhulumiwa,” akasema.

Mbali na kupigwa, wanafunzi hao hutukanwa na wanaume hao na jamii hali ambayo inawadhalilisha.

Bi Yusuf alisema ipo haja kwa serikali ya kaunti na ya kitaifa pamoja na mashirika kuwahamasisha wanafunzi hawa kuhusu dhuluma ya kijinsia.

Alieleza kuwa chuo cha Pwani kiko tayari kufanya mikataba na mashirika yasiyo ya serikali na kutatua changamoto zitakazosaidia kuzuia dhuluma za jinsia.

“Wavulana pia wanapitia dhuluma za jinsia. Wao hupigwa na hudungwa visu kutokana na mizozo ya mapenzi lakini hawataki kupiga ripoti kwa polisi,” akasema.

Hata hivyo, aliwakosoa baadhi ya wanafunzi kwa kutotilia maanani mikakati ya chuo hicho kutaka kutatua changamoto ya umaskini.

“Baadhi ya wanafunzi hupewa kazi ndogondogo kama kufanya usafi katika chuo ili kupata pesa za matumizi lakini wanakosa kuendelea baadaye,” akasema.

You can share this post!

Jumwa asisitiza azma yake ya ugavana Kilifi bado haijafa

SHINA LA UHAI: Hofu magonjwa ya mdomo yakiongezeka nchini

T L