Habari za Kaunti

Hofu watoto wanaoambukizwa Ukimwi na mama zao wakiongezeka

March 31st, 2024 1 min read

NA ERIC MATARA

MAAFISA wa afya katika Kaunti ya Narok wameelezea wasiwasi kuhusu ongezeko la idadi ya watoto wanaoambukizwa virusi vya HIV kutoka kwa mama zao eneo hilo.

Takwimu mpya kutoka Idara ya Afya ya Kaunti zinaashiria kuwa maambukizi ya HIV – ambayo husababisha Ukimwi- ni asilimia 21.1 zaidi ya kiwango cha jumla nchini cha asilimia nane.

“Kiwango cha maambukizi ya Ukimwi Narok kimepita kiwango cha kitaifa,” ilisema ripoti ya idara.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, eneo la Trans Mara Magharibi ndilo limeathirika zaidi likiongoza kwa asilimia 31.4 ya maambukizi.

Narok Kaskazini ni asilimia 21.4, Narok Kusini, (asilimia 18.8) Narok Magharibi (asilimia 17.1) na Narok Mashariki (asilimia 13.5).

Mshauri wa kinga dhidi ya Ukimwi, Narok Kaskazini, Purity Kisaka, alisema idadi ya juu ya maambukizi inachangiwa hasa na wazazi wasio na ufahamu ambao hawajitokezi kupimwa wakati wa vipindi vya kliniki huku wengine wakikosa kutumia dawa wamavyoagizwa na madaktari.

“Idadi kubwa ya visa inahusisha kina mama wanaokosa kujitokeza kwa vipimo wakati wa vipindi vya kliniki. Tunawahamasisha wanawake wajawazito na wanandoa katika kila kijiji ili kuwapa motisha wa kupimwa kuhusu maradhi,” alisema Bi Kisaka.

“Mara nyingi unakuta kina mama wakienda kliniki pekee yao bila waume zao. Anapopatikana bila virusi, mume wake anafikiri yupo salama ilhali huenda ana mipango ya kando ambao huenda wanaugua gonjwa hilo.”