Hofu ya Eunice Sum kuhusu kufifia kwa kina dada Wakenya mbio za mita 800

Hofu ya Eunice Sum kuhusu kufifia kwa kina dada Wakenya mbio za mita 800

Na GEOFFREY ANENE

ZAIDI ya miaka mitano tangu ashinde medali yake ya mwisho, bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 mwaka 2013 Eunice Sum ameelezea wasiwasi wake kuhusu Kenya kupoteza umaarufu katika kitengo hicho cha kuzunguka uwanjani mara mbili.

Katika mahojiano na Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K), Sum, 33, ambaye anajiandaa kustaafu kushiriki mbio za mita 800, alisema, “Natumai kuwa hivi karibuni Shirikisho la Riadha Kenya (AK) na wadau wanaojishughulisha na riadha, watawekeza zaidi katika talanta chipukizi ili kuziba pengo linaloachwa katika mbio za mita 800.”

Kenya imewahi kutwaa taji la mbio za mita 800 za kinadada kupitia Pamela Jelimo kwenye Olimpiki 2008 na Riadha za Dunia za Ukumbini 2012 na Janeth Jepkosgei na Sum katika Riadha za Dunia mwaka 2007 na 2013, mtawalia. Pia, ilinyakua taji la Jumuiya ya Madola kupitia kwa Jepkosgei (2006), Nancy Langat (2010) na Sum (2014).

Aidha, Sum amesema amejawa na ari kuhusu kurejea kwenye Olimpiki anapojiandaa kuwakilisha Kenya jijini Tokyo, Japan.

Licha ya kuwa michezo hiyo itafanyika katikati ya janga la Covid-19, Sum amesema yuko tayari kwa mashindano.

“Kujiandaa kwa Olimpiki kumekuwa na changamoto zake, hasa kufanya mazoezi peke yako wakati wa janga la Covid-19,” alisema.

Alifichua kuwa lengo lake kubwa kwanza jijini Tokyo ni kufuzu kushiriki fainali.

“Mbio zangu ni mchezo unaohitaji mtu kuwa makini. Lengo langu kwanza ni kufuzu kushiriki fainali halafu nitajipanga vyema kwa fainali,” alisema Sum.

Mtimkaji huyo alidai kuwa kukosekana kwa majina makubwa kama vile bingwa mtetezi Caster Semenya kumefungulia mlango yeyote kutwaa taji.

“Bado Wakenya tutapata ushindani mkali kwa sababu Olimpiki ina kizazi kipya cha washiriki,” alikiri Sum ambaye alifuzu pamoja na Wakenya wenzake Mary Moraa na Emily Tuei kushiriki Olimpiki zitakazoandaliwa jijini Tokyo kutoka Julai 23 hadi Agosti 8.

  • Tags

You can share this post!

IEBC imeainisha wazi mazingira ya kituo cha kura –...

Shujaa yafunzwa umuhimu wa utimamu wa kiakili nao Lionesses...