Habari

Hofu ya ghasia Amerika

November 4th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

HOFU ya mapigano kutokea Amerika baada ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumanne imekumba raia wengi wa nchi hiyo huku wengi wakichukua hatua za kujihakikishia usalama wao na mali yao.

Wafuasi wa Rais Donald Trump wa chama cha Republican na mpinzani wake wa chama Democratic, Joe Biden, walieleza kuwa kuna uwezekano wa kulipuka kwa ghasia matokeo ya uchaguzi yatakapotangazwa rasmi.

Katika miji mingi kote Amerika, biashara zimefungwa na kuongezewa milango ya usalama kuzuia kuvunjwa na mali kupororwa iwapo ghasia zitazuka. Ni taswira ambayo wengi wanahusisha na mataifa mengi ya Afrika ambapo ghasia za baada ya uchaguzi ni jambo la kawaida.

Wafuasi wa Biden wanashuku huenda Rais Trump asikubali kung’atuka mamlakani iwapo atashindwa kwenye uchaguzi huo.

Hofu hii ilitanda baada ya usalama katika ikulu ya White House kuimarishwa kwa kuzungushwa ua maalumu ili kuzuia watu kuikaribia.

Duru zinasema kwamba ua huo ambao ulianza kuwekwa Jumatatu utadumu kwa siku kadhaa baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.

Hatua ya kuweka ua huo ilitokana na ushauri wa shirika la ujasusi la Amerika (CIA), ishara kwamba lina habari za kuaminika za uwezekano wa ghasia kulipuka nchini humo.

“Huduma ya ujasusi ilionya na kushauri kuwa watu wanafaa kuzuiwa kutembelea maeneo yaliyo karibu na White House kwa muda kama njia moja ya kuimarisha usalama wakati wa uchaguzi wa urais, kulinda na kudumisha usalama wa umma,” ilisema taarifa ya idara ya kulinda maeneo ya umma.

Maafisa wa usalama kote Amerika pia wamechukua hatua za kukabili fujo zikizuka kwa kufanya mazoezi na kuanzisha vituo vya kuzidhibiti.

Maandalizi ya kukabili ghasia za baada ya uchaguzi yalianza mapema huku maafisa wa uchaguzi wakipatiwa mafunzo ya kujihakikishia usalama.

Afisa wa uchaguzi jijini Naperville, Illnois Ellen Sorensen, aliambia gazeti la Washington Post kwamba, wakati huu kuna uwezekano wa kuzuka kwa ghasia.

“Hatujakuwa na hofu katika chaguzi za awali, lakini wakati huu, tunaweza,” alisema.

Kundi la Election Protection, jimbo la Arizona lilisema kuwa, limefunza mamia ya watu kuhusu jinsi ya kujilinda na kuepuka fujo za uchaguzi.

Kura za maoni kabla ya tarehe ya Jumanne zilionyesha Biden aliongoza kwa umaarufu lakini Trump alizipuuza.

Rais huyo pia alilalamikia upigaji kura wa mapema na kwa njia ya posta akisema ungetumiwa kuvuruga matokeo ya mwisho.

Mnamo Juni, alinukuliwa akipendekeza uchaguzi kuahirishwa hatua iliyopingwa vikali hata na wabunge na maseneta wa chama chake cha Republican.

Dalili za fujo zilianza kuonekana mapema kufuatia hatua ya Trump ya kutumia walinda usalama kukabiliana na waandamanaji waliolalamikia mauaji ya watu weusi nchini humo.

Mnamo Jumatano wiki jana, Biden alilazimika kufuta mkutano wa kampeni Texas wafuasi wa Trump walipozingira basi lake.

Kote Amerika, misafara ya wafuasi wa Trump imekuwa ikiteka na kudhibiti barabara kuu na madaraja huku wakitisha wafuasi w Biden.

Msafara mmoja ulionekana Marin City, jimbo la California, ambako Waamerika weupe ni wachache huku wakiropokwa matamshi ya kuchochea ubaguzi wa rangi.

Katika mji wa Fort Worth, msafara mwingine wa wafuasi wa Rais huyo ulipitia karibu na kituo cha kupigia kura katika mtaa wanaoishi Waamerika wenye asili ya Kiafrika ambao wanamuunga Biden hatua iliyozua malumbano.

Gazeti la HuffingtonPost liliripoti kuwa katika mji wa Temecula, California, msafara wa wafuasi wa Trump ulifunga kituo cha kupigia kura na katika jiji la Louisville, Kentucky, mfuasi Trump aliongoza magari akishika bunduki.

Kulingana na gazeti hilo, misafara hiyo iliongozwa na kundi linalotetea Waamerika weupe katika juhudi za kutisha watu.

“Ni wakati wa kusimama na kujirudishia nchi yetu,” kundi hilo lilisema kwenye tovuti yake.

Wafuasi wa Biden wanasema kwamba, taharuki ambayo imetanda Amerika imechochewa na matamshi ya Trump yanayoonyesha huenda asikubali matokeo iwapo atashindwa.