Habari Mseto

Hofu ya maafa mgomo ukichacha

December 22nd, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MAAFA yanawakodolea macho wagonjwa nchini baada ya wahudumu wa afya wanaogoma kuacha hospitali na vituo vya afya vya umma vikiwa mahame.

Wagonjwa waliofika katika vituo hivyo kote nchini walisononeka kwa maumivu bila wa kuwahudumia huku walinzi wakiwaagiza kutafuta huduma katika hospitali za kibinafsi.

Madaktari walioanza mgomo jana, waliungana na wauguzi na matabibu kusema hakuna vitisho vinakavyowafanya kufuta mgomo huo kabla ya matakwa yao kutimizwa.

“Hakuna vitisho vitakavyofanya madaktari kurudi kazini. Maagizo ya mahakama hayatazuia madaktari kufariki au kuambukizwa maradhi,” alisema kaimu Katibu Mkuu wa chama cha Madaktari na wataalamu wa meno (KMPDU) Dkt Chibanzi Mwachonda alipozindua rasmi mgomo huo mjini Kisii.

Mnamo Jumamosi, waziri wa afya Mutahi Kagwe aliwalaumu wahudumu wa afya kwa kugoma licha ya mahakama kuharamisha mgomo wao na kuagiza serikali za kaunti kuwafuta kazi.

Dkt Mwachonda alitaja kauli hiyo kama vitisho na kuingiza siasa katika masuala ya afya.“Madaktari nchini Kenya hawawezi kusubiri, hawawezi kuendelea kuhudumu katika mazingira hatari,” alisema.

Katika hospitali ya rufaa ya Pwani, wagonjwa waliofika kutafuta huduma za dharura waliagizwa kwenda katika hospitali za kibinafsi, jambo ambalo ni mlima kwa Wakenya wengi wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na athari za janga la corona.

Hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi huku maambukizi ya virusi vya corona yakiendelea kuongezeka nchini.Mkurugenzi wa huduma za uuguzi katika hospitali ya rufaa ya Pwani , Elizabeth Kivuva alidai wameajiri madaktari na wauguzi kwa kandarasi kusaidia kukabiliana na mzozo huo.

“Tunashughulikia wagonjwa wa corona pekee. Wengine wote wanahamishwa,” alisema.Katika kaunti ya Tana River, wagonjwa na akina mama wajawazito waliachwa katika wodi bila wahudumu wa kuwashughulikia.

Baadhi waliweka maisha yao hatarini kwa kutafuta huduma za wakunga wa kitamaduni kwa kukosa pesa za kwenda hospitali za kibinafsi.

“Nilikuja hapa na nikapata milango yote imefungwa, hakuna daktari au muuguzi hata mmoja,” alisema Mwanaharusi Jillo. Wagonjwa wa figo waliofika kusafishwa damu walisononeka wasijue pa kuelekea.

Katika kaunti ya Kilifi, hakuna hospitali ya umma iliyokuwa ikipokea wagonjwa. Baadhi ya walioonekana kupata nafuu waliruhusiwa kuondoka wodi hata kabla ya kupona.

Mwenyekiti wa tawi hilo la KMPDU, Dkt Sammy Kiptoo alisema kwamba, madaktari hawatarudi kazini matakwa yao yasipotimizwa.Huduma za afya katika kaunti ya Taita Taveta, pia zililemazwa huku maafisa wa chama hicho wakisema hawatarudi kazini.Hali ilikuwa sawa katika kaunti ya Lamu wagonjwa wakisononeka kwa kukosa huduma.

Wagonjwa wanaotafuta huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Uasin Gishu walitaabika wakitafuta matibabu bila wa kuwahudumia.

Mwanamke mwenye umri wa makamo ambaye alikuwa akitafuta huduma kujifungua mtoto alisema alielekezwa na walinzi kutafuta huduma kwingine.Doreen Rotich ambaye anatarajia mtoto wakati wowote aliomba magavana na serikali ya kitaifa kuingilia kati.

‘Nilikuja hapa mapema saa tatu asubuhi tangu wakati huo hakuna huduma ambazo nimepokea. Wafanyikazi wa pekee ambao tunakutana nao ni walinzi. Serikali zote za kitaifa na kaunti lazima zipate suluhisho la mgomo huu,”akasema Bi Rotich.

Mwenyekiti wa chama cha wauguzi kaunti ya Uasin Gishu, Francis Chekwony alisema hakuna huduma katika hospitali za kaunti.Hali ilikuwa sawa Elgeyo Marakwet ambapo zaidi ya wauguzi 600 na wahudumu wengine wa afya wamesusia kazi.

Katibu Mkuu wa tawi la kaunti hiyo la chama cha wauguzi, Benson Biwott alitaka viongozi wa kaunti hiyo kukoma kuwatishia wauguzi wanaogoma.

Ripoti za Ruth Mbula,Benson Matheka, Lucy Mkanyika, Maureen Ongalo, Kalume Kazungu, Stephen Oduor, Winnie Atieno, Titus Ominde