Hofu ya msambao mpya kanuniza kudhibiti corona zikipuuzwa

Hofu ya msambao mpya kanuniza kudhibiti corona zikipuuzwa

Na BENSON MATHEKA

WANASIASA wa vyama vikuu katika chaguzi ndogo za maeneobunge ya Juja Kaunti ya Kiambu, Bonchari, Kaunti ya Kisii na wadi ya Rurii Kaunti ya Nyandarua, wamekuwa wakikaidi kanuni za kuzuia msambao wa corona wakifanya kampeni.

Mapuuza ya viongozi hao yanajiri huku wataalamu wakionya kwamba kuna hatari ya nchi kukumbwa na wimbi la nne la virusi hivyo kuanzia Julai mwaka huu.

Wanasiasa wa vyama vya Jubilee, United Democratic Alliance (UDA) na Orange Democratic Movement (ODM), wamekuwa wakiandaa mikutano ya hadhara ambayo imepigwa marufuku.

Alipolegeza masharti ya kudhibiti corona Mei 1 mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta alidumisha marufuku ya mikutano ya siasa kote nchini. Hata hivyo, wiki hii viongozi wa chama cha UDA wakiongozwa na mbunge wa Kandara, Bi Alice Wahome waliandaa mikutano kadhaa eneo la Bonchari kupigia debe mgombeaji wa chama hicho, Bi Teresa Bitutu.

Katibu Mkuu wa chama cha ODM, Bw Edwin Sifuna pia alifanya mikutano kadhaa kumpigia debe, Bw Parvel Omeke. Mnamo Alhamisi, Gavana wa Kaunti hiyo, Bw James Ongwae pia alilalamika kuwa polisi walivamia boma lake kwa madai ya kutawanya mkutano haramu.

Katika wadi ya Rurii, Gavana wa Nyandarua aliandaa mkutano kumpigia debe mgombeaji wa chama cha Jubilee, Bw Peter Thinji naye mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro akaongoza ujumbe wa UDA kurai wapiga kura kumchagua mwaniaji wa chama hicho, Bw Francis Muraya.

Mnamo Alhamisi, wizara ya afya ilionya kuwa nchi itakumbwa na wimbi la tatu la janga la corona kuanzia Julai kufuatia kuthibitishwa kwa aina ya virusi vinavyosambaa India.

Wizara ilisema kwamba visa 20 vya virusi vinavyolemea India vimethibitishwa nchini.Mkurugenzi wa Afya, Dkt Patrick Amoth, alisema kwamba janga la corona lina mtindo ambao mkumbo mpya unatokea kila baada ya miezi mitatu.

Mnamo Machi, Kenya ilikumbwa na wimbi la tatu la janga la corona, wanasiasa pia wakiongekana kuchangia zaidi kwa kupuuza kanuni za wizara ya afya na kuandaa mikutano ya hadhara kupigia debe Mswada wa marekebisho ya Katiba wa BBI.

“Tunaweza kusema kwa hakika kwamba iwapo mtindo huu utaendelea, tutakuwa na mkumbo mwingine Julai,” alisema Bw Amoth.

You can share this post!

JAMVI: ‘Baba’ anajua kwamba UhuRuto wanamkata...

JAMVI: Mirindimo mipya ya Tangatanga baada ya BBI kuzikwa