Habari Mseto

Hofu ya msongamano feri mpya ikiharibika Likoni

July 22nd, 2020 2 min read

Na MOHAMED AHMED

HUENDA huduma katika kivuko cha Likoni zikatatizika baada ya feri mpya ya Mv Safari ambayo ni miongoni mwa zile kubwa nchini, kuharibika.

Feri hiyo ambayo ilinunuliwa pamoja na Mv Jambo kwa gharama ya Sh2 bilioni, imekuwa ikihudumu kwa kivuko hicho katika muda usiozidi miezi mitatu.

Feri hiyo iliharibika baada ya kugongwa na feri ya Mv Kwale Jumanne jioni.Ajali hiyo ilisababisha msongamano na mkanyagano katika kivuko hicho mnamo Jumanne kwa kuwa idadi ya feri zinazohudumu ilikuwa imepungua.

Watu 18 walijeruhiwa katika tukio hilo na kupekejkwa hospitali kuu ya Pwani kwa matibabu.

Idadi hiyo iliongezeka baada ya watu 13 kuripotiwa awali kuumizwa kwenye msongamano huo uliotokea katika upande wa Mombasa kisiwani JumanneJana, Taifa Leo ilithibitisha kuwa baadhi ya waliojeruhiwa ambao walikuwa ni wanawake, waliruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kupata nafuu.

Usimamizi wa Shirika la Huduma za Feri (KFS), ulieleza kuwa feri hiyo ya Mv Safari ilitoboka upande mmoja baada ya kugongwa na feri ya Mv Kwale.

Ajali hiyo ambayo ilitokea upande wa Likoni ilisababisha maji kuingia ndani ya injini ya feri hiyo na kuikwamisha isiweze kuendeleza shughuli zake.

“Kwa sasa tunaishughulikia feri hiyo kwa kutoa maji yaliyoingia kwenye injini. Tundu hilo litazibwa mara tu maji hayo yakitolewa,” akasema meneja mkurugenzi wa huduma hizo, Bw Bakari Gowa, katika taarifa fupi kwa wanahabari.

Kufikia jana asubuhi, feri hiyo ilikuwa bado inashughulikiwa na kufanyiwa ukarabati na wahandisi wa KFS.Hata hivyo, shirika hilo liliweka feri nne jana asubuhi kuhudumia wasafiri.

Ingawa hatua hiyo ilisaidia uchukuzi, kuondolewa kwa Mv Safari bado kutatiza huduma hasa nyakazi za jioni. Feri hiyo imekuwa ikichangia pakubwa kupunguza msongamano kwa sababu ina nafasi kubwa ya kubeba watu na magari.

Feri hiyo inaweza kubeba watu 1,500 na magari 62 kwa safari mojha, kulingana na kampuni ya Ozata Shipyard, iliyoiunda.

KFS inamiliki feri saba kwa jumla ikiwemo hiyo ya Mv Safari, Mv Jambo, Mv Kwale, Mv Likoni, Mv Kilindini, Mv Harambee na Mv Nyayo.Feri ya Mv Nyayo pia imekuwa ikifanyiwa ukarabati baada ya kuondolewa majuzi.

Pia feri ya Mv Harambee iliondolewa baada ya kuhusika katika ajali mwaka jana, ambapo gari lilitumbukia kwa maji na kusababisha kifo cha mama na mwanawe.