Michezo

Hofu ya Shujaa baada ya raga ya Afrika kufutiliwa mbali

June 10th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Kevin Wambua, amesema kwamba kufutiliwa mbali kwa msimu wa Raga ya Afrika ni pigo kubwa kwa kikosi chake ambacho hutegemea mapambano ya humu barani kuwaweka wachezaji wake kwenye mizani.

Shujaa ambao ni mabingwa wa bara la Afrika, sasa hawatatetea ufalme wao waliojinyakulia jijini Johannesburg, Afrika Kusini mwaka 2019 baada ya fainali za mwaka 2020 kutupwa kutokana na janga la corona.

Wambua wanaraga wake sasa watakosa fursa ya kupimana ubabe na miamba wenzao kutoka humu barani.

“Ni fursa ambayo tutaikosa kwa sababu tumekuwa tukitumia mashindano hayo kuwapa wanaraga wetu chipukizi majukwaa ya kujipima uwezo katika ulingo wa kimataifa.”

Ingawa hivyo, Shujaa watapata fursa ya kunogesha duru nne za mwisho za Raga ya Dunia msimu huu jijini London na Paris mnamo Septemba kabla ya kutua Singapore na Hong Kong mnamo Oktoba, 2020.

Wambua amewataka wakufunzi wa klabu za raga za humu nchini kubuni mikakati kabambe itakayowapa wachezaji wao fursa maridhawa za kujifua vilivyo wakati huu wa ugonjwa wa Covid-19.

“Ipo haja kwa makocha wa klabu za Kenya Cup na Championship kufikiria uwezekano wa kubuni mbinu mpya za kuwashughulisha wachezaji kimazoezi ili wasiwe wamepoteza fomu wakati wa kurejelewa kwa mashindano. Hili litawaepushia pia wanaraga majeraha mabaya ya mara kwa mara ambayo huenda yakagharimu kabisa taaluma zao,” akasisitiza.

Chini ya kocha Felix Oloo, kikosi cha taifa cha wanaraga wa kike, Kenya Lionesses pia walikuwa wameratibiwa kuvaana na Colombia katika juhudi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.

Wanaraga wa 7’s walikuwa wamepangwa kushiriki pia mchujo wa kufuzu kwa Raga ya Dunia nchini Afrika Kusini kabla ya kunogesha duru ya Langford Sevens nchini Canada.