Hofu ya siasa za urithi kutawala Mashujaa Dei

Hofu ya siasa za urithi kutawala Mashujaa Dei

Na VALENTINE OBARA

SIASA za urithi wa urais mwaka wa 2022 zinahofiwa kuteka sherehe za Mashujaa Dei hii leo Jumatano katika Kaunti ya Kirinyaga, huku joto la kisiasa linapozidi kuenea nchini.

Hii itakuwa ni sherehe ya mwisho ya Mashujaa kuongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, atakayekamilisha kipindi chake cha urais mwaka 2022.

Vigogo wakuu wa kisiasa ambao wanamezea mate urithi wa urais mwaka 2022 wanatarajiwa kukutana katika hafla hiyo ya kitaifa.

Joto la kisiasa tayari liliamshwa kufuatia ziara za Kiongozi wa ODM, Raila Odinga na Rais Kenyatta, ambao walifanya mikutano tofauti ya hadhara katika maeneo ya Kati wiki hii.

Viongozi wengine wanaotarajiwa katika hafla hiyo ni Naibu wa Rais William Ruto, na vinara wa Muungano wa One Kenya Alliance (OKA) ambao ni Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Mwenyekiti wa KANU aliye pia Seneta wa Baringo Gideon Moi, na Seneta wa Bungoma, Moses Wetang’ula anayeongoza Ford Kenya.

Rais Kenyatta amezidi kuonyesha ishara kuwa ataunga mkono azimio la Bw Odinga katika uchaguzi ujao, wandani wake wakidai Dkt Ruto alimsaliti alipomkaidi kama vile alipopinga Mpango wa Maridhiano (BBI).

Kwa mara ya pili katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja, Rais Kenyatta aliashiria hayo alipohutubia wananchi alipokuwa katika msafara Jumatatu baada ya kukutana na viongozi wa Kaunti ya Kirinyaga.

Katika hotuba yake, Rais aliwasifu wakazi wa Mlima Kenya kwa kumkaribisha vyema “mgeni” wake, akionekana kumrejelea Bw Odinga, huku akiwaonya dhidi ya wanasiasa ambao hakuwataja aliodai wanataka kuwadanganya.

“Kuweni makini na yale ambayo wanakuja kuwaambia. Wakija na pesa, chukueni lakini ifikapo wakati wa uchaguzi fanyeni maamuzi kwa busara,” akasema.

Kura za eneo la Kati zimevutia wanasiasa wanaopanga kuwania urais 2022, ikizingatiwa kuwa kuna matarajio hapatakuwepo mgombeaji urais wa kutoa wengine jasho kutoka eneo hilo.

Katika ziara zake, Dkt Ruto hulaumu BBI kwa kuathiri utekelezaji wa miradi ya serikali wakati wa kipindi cha pili cha uongozi wa Jubilee, huku akitumia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho kujinadi kwa wananchi.

“Viongozi hawa wengine wanaotaka kuungwa mkono na Rais walimtoroka wakati alipowahitaji. Mimi pekee ndiye niliyesimama naye imara,” Naibu Rais alisema, alipokuwa katika ziara ya kaunti za Pwani aliyokamilisha Jumanne.

Kando na siasa, wananchi wengi wanatazamia kuona kama serikali itatangaza mpango wowote mpya wa kuwafaidi kimaisha.

Katika siku za hivi majuzi, kumekuwa na malalamishi mengi kuhusu kiwango cha juu cha ushuru wa mafuta ambacho kinafanya bei ya mafuta iwe ya juu kupita kiasi.

Hali hii imeongeza ugumu wa maisha ambao ulikuwa tayari umepanda tangu wakati janga la corona lilipotangazwa nchini mwaka 2020.

Kufikia Jumanne, baadhi ya kanuni zilizonuiwa kuepusha maambukizi ya janga la corona zilikuwa zinaendelea kutumiwa ikiwemo kafyu na masharti yanayoathiri shughuli za maeneo ya ibada na yale ya starehe.

You can share this post!

Agizo la Joho kuhusu miraa lapingwa vikali

Sherehe zatuliza vita vya ubabe Kirinyaga

T L