NA ANTHONY KITIMO
WAKAZI wa mtaa wa Tudor, Kaunti ya Mombasa, wameeleza wasiwasi kuhusu ongezeko la ujenzi wa majumba ya ghorofa karibu na Bahari Hindi.
Mwenyekiti wa Muungano wa Wakazi wa Tudor Nora, Bw Shakeel Khan, alisema juhudi zao za kutaka ujenzi usitishwe hazijafua dafu.
“Mikoko kadha ambayo tumekuwa tukitunza katika sehemu ya bahari, imekatwa,” akasema.
Wakazi hao walieleza wasiwasi kuhusu uwezekano wa uchafuzi wa bahari.
Diwani wa Tudor, Bw Samir Balo, alisema atawasilisha suala hilo katika bunge la kaunti kwani kuna hatari iwapo ujenzi huo ni haramu.
Wiki chache zilizopita, Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, alitoa ripoti ya uchunguzi uliobainisha kuna majengo 97 yanayoendelezwa bila idhini ya serikali ya kaunti.
Alisema kuwa, baadhi ya majengo yalikuwa yameagizwa kusitishwa ilhali wawekezaji walipatikana bado wanaendeleza ujenzi.
Subscribe our newsletter to stay updated