Hofu ya wanavijiji kumiliki silaha kali Kapedo

Hofu ya wanavijiji kumiliki silaha kali Kapedo

FLORAH KOECH na BARNABAS BII

HATUA ya baadhi ya wapiganaji kwenye mzozo unaohusisha jamii za wafugaji eneo la North Rift kumiliki silaha za kisasa imeathiri juhudi za viongozi kuleta amani kwenye mpaka wa kaunti za Baringo na Turkana.

Isitoshe, maafisa wa usalama pia wamekuwa na wakati mgumu kupambana na visa vya wizi wa mifugo na migogoro ya mipaka.

Shughuli za kiuchumi zimeathirika katika maeneo ya mpaka kati ya kaunti hizo mbili baada ya wavamizi wenye silaha kufanya mashambulio ya kulipiza kisasi haswa eneo la Kapedo.

Licha ya makataa yaliyotolewa na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i miaka miwili iliyopita kwamba watu wanaomiliki bunduki kinyume cha sheria wazisalimishe, bunduki haramu zingali zinaingizwa eneo la Kapedo, kupitia Bonde la Kerio.

Mnamo Jumanne, taharuki ilipanda katika eneo hilo baada ya wavamizi wanaoshukiwa kutoka jamii ya Pokot kumuua mfugaji kutoka jamii ya Turkana kwa kumpiga risasi na kuwajeruhi wafugaji wengine wanne.

Mamia ya familia zimehama makwao kufuatia shambulio hilo na kikosi cha walinda usalama kimetumwa kutuliza uhasama kat ya jamii hizo hasimu za Turkana na Pokot.

Shughuli za masomo zimeathirika huku shule zikisalia mahame baada ya wanafunzi kuondolewa kufuatia mashambulio hayo ambayo pia yalihusisha uteketezaji wa nyumba kadha.

Miongoni mwa shule zilizoathirika ni Shule ya Upili ya Kapedo, Shule ya Msingi ya Kapedo, Shule ya Msingi ya Wasichana ya Kapedo, Shule ya Msingi ya Lomelo na Shule ya Msingi ya Silale.

Wanafunzi walioathirika wamelazimika kuishi katika manyatta zilizoko viungani mwa kituo cha kibiashara cha Kapedo. Hii ni kwa sababu shughuli za uchukuzi katika eneo hilo zimekwama ingawa magari ya polisi yanashika doria katika eneo hilo.

Shughuli za uchukuzi kati ya barabara za Kapedo- Marigat na Kapedo- Lomelo zimeathirika kwa sababu wakazi wanaogopa kushambuliwa na wahalifu hao wanaaminika kujificha katika misitu ya karibu.Bi Evaline Ekaudu, mmoja wa wakazi alisema anaogopa kutoka nyumbani asije akashambuliwa na wahalifu hao wenye silaha hatari ambao wanazunguka huko licha ya kuwepo kwa polisi eneo hilo.

Wakazi hao wanakabiliwa na hatari ya kuathirika na njaa kwa sababu wao hupata vyakula kutoka mji wa Marigat ulioko eneo bunge la Baringo Kusini.

“Tuna hofu kwamba wakazi watakufa njaa ikiwa hatua ya haraka haitachukuliwa kukabiliana na kero hili la ukosefu wa usalama. Vyakula huletwa kutoka Marigat lakini sasa hakuna magari yanatoka huko kuja hapa. Vile vile, watu kutoka hapa hawawezi kuenda Lokori kwa sababu wakora wanaaminika kujificha kando ya barabara ya Kapedo–Lokori,” akasema Bi Ekaudu.

You can share this post!

MAUYA OMAUYA: Usitarajie mabadiliko Kenya mwaka huu

Mbunge wa zamani kortini kwa wizi wa shamba