Hoki: Mechi 3 kupigwa Jumapili

Hoki: Mechi 3 kupigwa Jumapili

Na JOHN KIMWERE

JUMLA ya mechi tatu za magongo kwa upande wa wanaume katika Ligi Kuu zimeratibiwa kuchezwa Jumapili uwanjani City Park, Nairobi.

Wafalme wa mchezo huo, Butali Warriors na mahasimu wao Kenya Police kila moja itakuwa kazini kuwinda alama tatu muhimu kupigania kumaliza mechi za mkumbo wa kwanza kwa ushindi.

Maafande wa Kenya Police chini ya kocha, Patrick Mugambi wataingia mzigoni kucheza na Sailors huku wakilenga kufanya kweli. Nayo Butali Warriors imepangwa kukabili Wazalendo ikipania kuvuna pointi tatu na kumaliza mkumbo wa kwanza ikiwa kileleni mwa jedwali.

“Tumepania kupambana mwanzo mwisho dhidi ya wapinzani wetu nia yetu ikiwa kuwazima na kubeba alama zote tatu ili kujiweka pazuri kutwaa taji la muhula huu,” kocha wa Police, Patrick Mugambi amesema na kutoa wito kwa vijana wake kutolaza damu dimbani.

Police inajivunia huduma za wachezaji kama Oliver Echenje, Victor Wekesa, Titus Kimutai, Derrick Jabali, Brian Saina na Samuel Oungo kati ya wengine.

”Kiukweli tunafahamu wazi kuwa tunatarajia kibarua kigumu lakini tumejipanga kukabili wapinzani bila hofu huku tukilenga kuzoa alama zote tatu,” nahodha wa Butali, Constant Wakhura amesema.

Nayo timu ya Mashujaa ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha USIU itashuka dimbani kukutanishwa na Greensharks.

Kwenye msimamo wa kipute hicho, Butali Warriors inaongoza kwa kuzoa alama 20, moja mbele ya Kenya Police baada ya kila moja kushiriki mechi nane.

Wanazuo Gladiators kutoka Chuo Kikuu cha Strathmore wanashikilia nafasi ya pili kwa kusajili pointi 13, mbili mbele ya Wazalendo sawa na Sailors tofauti ikiwa idadi ya mabao.

  • Tags

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Siku 10 za mwanzo za mwezi muhimu wa...

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Madola waanza nchini Rwanda

T L