Hoki: Titans yajipatia miaka 5 ili kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Afrika  

Hoki: Titans yajipatia miaka 5 ili kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Afrika  

NA JOHN KIMWERE 

TIMU ya warembo ya mpira wa magongo ya Titans ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) imekaa pazuri kujikatia tiketi ya kufuzu kupanda kushiriki Ligi Kuu muhula ujao.

Vipusa hawa wa kocha, Richard Wandera ni kati ya vikosi saba vinavyoshiriki ngarambe ya Supa Ligi msimu huu.

“Sina shaka kutaja kuwa tunapambana mwanzo mwisho kwenye kampeni za muhula huu kuhakikisha tunajikatia tiketi ya kupanda ngazi msimu ujao na kurejea kushiriki Ligi juu tulioshushwa misimu miwili iliyopita,” kocha huyo amesema na kuongeza kuwa licha ya kuweka azma hiyo wanakabiliwa na mtihani mgumu.

Anafunguka kuwa licha ya kuwa wanafanya vizuri kwenye kampeni za kipute cha muhula huu lazima wajitume kiume ili kuzuia wapinzani wao wasiwapiku.

Mchezaji wa KU akiwa uwanjani. PICHA | JOHN KIMWERE

Anataja kuwa vikosi vya Mombasa Sports Club (MSC) na Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) vinakuja kivingine.

Hata hivyo anasema kuwa haitakuwa rahisi wamepania kupambana mwanzo mwisho kukabili wapinzani wao.

Kwenye msimamo wa kinyang’anyiro hicho, KU inaongoza kwa kufikisha alama 16 baada ya kushuka dimbani mara sita.

Nayo MSC ambayo imeshiriki mechi nne inashikilia nafasi ya pili kwa kuzoa pointi tisa, moja mbele ya UoN sawa na wanazuo wa Jomo Kenyatta (JKUAT) baada ya kushiriki mechi nne na tano mtawalia.

Kwenye ligi kuu Titans inajivunia kuwahi kumaliza nafasi ya sita.

Kocha huyo anafuraha tele kwa kutoa mchezaji mmoja, Gaudencia Ochieng  aliye katika kikosi cha taifa almaarufu Blades iliyosafiri nchini Uingereza kushiriki pambano la Michezo ya Jumuiya ya Madola.

Katika mpango mzima kocha huyu anasema ndani ya miaka mitano ijayo wanalenga kuibuka malkia wa Ligi Kuu na kujikatia tiketi ya kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Afrika (CCCA).

Kwenye michezo ya Ligi ya Vyuo Vikuu vya Kenya (KUSA) vichuna wa KU ni kati ya vikosi ambavyo hushusha ushindani mkali.

Mchezaji wa KU (kushoto) akishindana na mwenzake wa JKUAT. PICHA | JOHN KIMWERE

KU hushiriki mechi za Kanda ya Nairobi na inajivunia kuibuka malkia wa kipute hicho mwaka 2020 kwani imekuwa ikitinga fainali za kitaifa tangu mwaka 2018.

Kocha huyo anashauri wachezaji wake kuwa makini zaidi na wawe wakijifunza mambo tofauti wakati wote wanaposhiriki mazoezi pia wanaposhiriki mechi yoyote iwe ya ligi au kuwania shindano lolote.

Pia anashauri wachezaji chipukizi kuwa ili kuhakikisha wameiva vizuri katika mchezo huo lazima wajitume mazoezini na kuwa tayari kujifunza mambo tofauti kila wakati.

Titans ina wachezaji wanaojitahidiu Bethsheba Williams (nahodha), Eddah Wakomo, Melody Nyagaka, Susan Okumu, Marion Wekesa, Gaudencia Ochieng, Monica Kitui, Agnes Mmbone, Miriam Mwangi, Laura Webala na Helga Ndinda. Pia wapo Ashley Nyakio, Rachael Ogari, Brenda Gikundi, Grace Mugure, Gloria Juma, Marcelyne Ochieno na Daphne Kirui.

  • Tags

You can share this post!

Wanavoliboli wa KU wajiandaa kushiriki voliboli ya Kombe la...

STAA WA WIKI: Malkia mpya wa mbio za mita 5,000 anayefuata...

T L