Makala

HONGO BUNGENI: DCI na EACC kuchunguza wabunge wanaodaiwa kumeza hongo

November 21st, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya Bunge kuhusu Mamlaka na Hadhi sasa inazitaka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuchunguza madai kwamba baadhi ya wabunge walihongwa kuangusha ripoti kuhusu sakata ya uagizaji sukari ya magendo kutoka nje.

Hii ni baada ya kamati hiyo kudai kwenye ripoti yake kwamba uchunguzi wake wa wiki tatu ulibaini kuna uwezekano wabunge hao walipokea au kupeana rushwa wakati wa mjadala kuhusu ripoti ya sakata ya sukari mna Agosti mwaka huu.

“Kwa misingi ya ushahidi ambao kamati hii ilipokea kutoka kwa wabunge waliofika mbele yake, ni bayana kuwa baadhi ya wabunge walihusika katika uovu wa aina fulani,” inasema ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni Jumanne jioni na Mbunge wa Limuru Peter Mwathi.

“Kwa hivyo DCI na EACC zinapasa kuwachunguza wabunge ambao huenda walipokea au kupeana hong hiyo. Uchunguzi huo sharti ukalimilishwe siku 90 baada ya kupitishwa kwa ripoti hii bungeni,” ripoti hiyo inaeleza.

Hata hivyo, hii itategemea ikiwa wabunge wataidhinishwa ripoti hiyo itakapojadiliwa kabla ya wabunge kwenda kwa likizo ndefu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Ilidaiwa kuwa wabunge hao walipewa hongo ya kati ya Sh10,000 na Sh20,000 kukataa ripoti hiyo ambayo ilipendekeza mawaziri Henry Rotich (Fedha), mwezake wa Masuala ya Afrika Mashariki (Adan Mohammed) na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Felix Koskei wachukuliwa hatua za kisheria kuhusiana na sakata hiyo ya sukari.

Ripoti hiyo iliandaliwa na kamati ya pamoja ya bunge kuhusu Biashara na Kilimo iliyoongozwa na Mbunge wa Kieni Kanini Kegan na mwenzake wa Mandera Kusini Ada Haji baada ya kuendesha uchunguzi wa mwezi mmoja kubaini chanzo cha uagizaji wa sukari ya magendo nchini mwaka jana.

Vile vile, paliibuka tetesi kwamba baadhi ya sukari hiyo ilikuwa na sumu ya zebaki na madini mengine ambayo ni hatari kwa maisha ya mwanadamu.

Kamati hiyo ya mamlaka inayoongozwa na Spika wa Bunge Justini Muturi ilisema kuwa ilifikia uamuzi wake baada ya kuchambua ripoti za magazeti, kanda za video kuhusu wabunge kadha waliofika mbele yake, rekodi ya matukio bungeni siku hiyo na kauli za moja kwa moja kutoka kwa wabunge waliofika katika vikao vya kamati hiyo.

Baadhi ya wabunge waliofika mbele ya kamati hiyo ni; Didmus Barasa (Kimilili), Simba Arati (Dagoreti Kaskazini), John Waluke (Sirisia), James K’Oyoo (Muhoroni) na  Godffrey Osotsi (mbunge maalum), Wengine walikuwa ni Gathoni Wa Muchomba (Mbunge Mwakilishi wa Kiambu), Jane Kihara (Naivasha), Fatuma Gedi (Mbunge wa Kaunti ya Wajir), Geofrey Odanga (Matayos) Rahab Mukani (Mbunge wa Nyeri) na David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki)

Bw Barasa alidai mbele ya kamati hiyo kwamba Bi Gedi alijaribu kumhonga kwa Sh10, 000 ambazo zilikuwa ndani ya bahasha, madai ambayo Mbunge huyo Mwakilishi wa Wajir alikana.

Na Bi Wamuchomba alidai kuwa aliwasikia wabunge wenzake wa kike wakijadiliana chooni jinsi alivyopokea hongo ili waangushe ripoti hiyo ya sakata ya sukari.