Makala

HONGO BUNGENI: Wa Muchomba asimulia wabunge walivyomumunya hongo chooni

September 26th, 2018 4 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE Mwakilishi wa Kiambu Gathoni wa Muchomba Jumanne alishikilia kuwa aliwasikia wabunge wenzake wa kike walielezea, wakiwa ndani ya choo bungeni, jinsi walivyopokea hongo ili kuangusha ripoti kuhusu sakata ya uagizaji wa sukari ya magendo mwezi Agosti.

Akihojiwa na Kamati ya Mamlaka na Hadhi ya Bunge inayochunguza madai hayo Bi Wa Muchomba alisema kuwa alianza kupata habari kuhusu hongo hiyo alipokuwa katika eneo la mankuli.

“Niliwaona wabunge wakiingia katika chumba fulani na kutoka huko wakiwa wachangamfu. Baadaye nilisikia mbunge mmoja akisema hivi: ‘wewe unaachwa, ingia pale ichukue yako;'” akasema.

Kamati ya BUnge kuhusu Hadhi na Mamlaka ikisikiza ushahidi kuhusu wabunge waliotajwa kupokea hongo ili kuangusha ripoti ya sukari. Picha/ Charles Wasonga

 

“Nilipigwa na mshangao na ndipo baadhi ya wabunge wa kike walielekea chooni. Mle ndani nilisikia wakipiga gumzo jinsi walivyopokea kati ya Sh10,000 na Sh30,000 kutoka kwa mwenzetu Bi Fatuma Gedi. Wengine walielezea jinsi walivyowachukulia wenzao… nilishanga sana,” akaambia Kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Bunge Justin Muturi.

Hata hivyo wanachama wa Kamati hiyo Jude Njomo (Kiambu Mjini), Peter Mwathi (Limuru) na Vincent Tuwei (Aldai) walipomtaka kuwatambua wabunge hao, alisema kuwa hangewatambua kutokana na sauti zao.

Vile vile, alifafanua kuwa hakuona mbunge yeyote akipeana au kupokea hongo, japo alishangazwa na gumzo ya rushwa aliyosikia kutoka kwa wabungeni wenzake, ndani ya choo na kwenye eneo la chakula.

Mbunge wa Lugari Ayuv Savulaalishwa kiapo kabla ya kutoa ushahidi wake Septemba 25, 2018. Picha/ Charles Wasonga

“Nilipigwa na butwaa kwamba wabunge wangepokea hongo ili kuangusha ripoti kuhusu sakata ya uuzaji wa sukari yenye magendo na yenye sumu. Hii ni aibu kubwa na kando na kuwa kitendo kinachoshusha hadhi ya asasi hii,” akasema Bi Wa Muchomba.

Wakati huo huo, Mbunge Mwakilishi wa Wajir Fatuma Gedi aliyehojiwa baada ya Bi Wa Muchomba alikiri kuendesha kampeni ya kuwashawishi wabunge waangushe ripoti hiyo kwa lengo la kuwanusuru mawaziri wawili aliolekezewa kidole cha lawama.

Alisema aliwashawishi wenzake baada ya kubaini kuwa ripoti hiyo haijibu swali la iwapo sukari ilikuwa na sumu ya zebaki bali iliwalaumu Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki Adan Mohamed na Henry Rotich (Fedha) “bila sababu yoyote”.

Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Wajir Bi Fatuma Gedi alipokiri kuwashawishi wenzake kuangusha ripoti hiyo. Picha/ Charles Wasonga

“Ndio niliwashawishi wenzangu kupinga hiyo ripoti kwa sababu mmoja wa waliolaumiwa Waziri Mohamed, anatoka eneo ninakotoka. Siasa huchezwa mashinani,” Bw Gedi akasema alipojibu swali kutoka kwa Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi aliyetaka kujua ikiwa “ushawishi” wake uliongozwa na hali kwamba mmoja wa mawaziri waliotajwa anatoka eneo lake.

Bi Gedi alisema hayo alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Mamlaka na Hadhi kujibu madai kwamba alijaribu kumhonga mbunge wa Kimilili Didmus Barasa kwa Sh10, 000 ili aangushe ripoti hiyo.

“Natoka kaunti ya Wajiri huku Waziri Mohamed akitoka kaunti jirani ya Mandera. Kando na hayo niliamini kuwa yeye na mwenzake Bw Henry Rotich wa Fedha hawakupasa kulaumiwa kwa sababu suala kuu lilikuwa ni iwapo sukari ilikuwa na zebaki au la; jibu ambalo lilifaa kutolewa na Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBs),” akaeleza.

Ripoti hiyo iliandaliwa na Kamati ya Pamoja ya Bunge kuhusu Kilimo na Biashara iliyooongozwa na Mbunge wa Kieni Kanini Kega na mwenzake wa Mandera Kusini Adan Ali.

Bi Gedi aliiambia kamati hiyo kwamba kabla ya madai hayo kuibuliwa hakuwa akimfahamu Bw Barasa “kwa sababu hatoki eneo ninakotoka.”

Mbunge wa Nakuru Mashariki David Gikaria alipopinga kuwahi kumshawishi mwenzake wa Naivasha Bi Jane Kihara kuangusha ripoti hiyo. Picha/ Charles Wasonga

“Nilipata habari hizo siku hiyo jioni nilipomwona kwenye runinga akidai kuwa nilijaribu kumpa bahasha iliyosheheni Sh10,000. Nilipigwa na butwaa kwa sababu dini yangu ya Kiislamu inapinga utoaji au upokeaji hongo,” akasema.

Vile vile, Bi Gedi aliiambia kamati hiyo, Bi Wa Muchomba alimhusishwa na uovu huo “kutokana na chuki za kibinafisi”.

“Wa Muchomba alinitaja kutokana na chuki ya kumshinda katika uchaguzi wa kundi la Wabunge 47 wanaowakilisha kaunti. Hizo ni chuki za kibinafisi ambayo zinapasa kupuuzwa na kamati hii,” akasema.

Bi Wa Muchomba aliiambia kamati hiyo kwamba alisikia wabunge wenzake wa kike wakielezea, wakiwa chooni, jinsi Bi Gedi alikuwa akiwahonga kwa kati ya Sh10,000 na Sh30,000 ili waangushe ripoti hiyo.

“Nilikuwa nimeenda chooni kwa haja na ndipo nikasikiwa baadhi ya wenzangu wa kike wakijadiliana jinsi walivyokuwa wamehongwa na Bi Gedi. Lakini sikuwatambua wala kuona wakihongwa,” akasema Bi Wa Muchomba huku akiongeza kuwa kitendo hicho kilishusha hadhi ya bunge.

Kamati hiyo itakamilisha uchunguzi wake mnamo Oktoba 3, 2018 kabla ya kuwaandaa ripoti yake. Bw Muturi alisema wabunge watakaopatikana na hatia wataadhibiwa kwa mujiu wa sheria.

Wengine walihojiwa na wanachama wa kamati hiyo ni; Ayub Savula (Lugari) na Joseph Tonui (Kuresoi Kusini) na David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki).

Bw Savula alidai wabunge walijaribu kusaka “vishawishi” kutoka kwa baadhi ya washukiwa ambayo walifika mbele ya Kamati hiyo ya pamoja, akitoa mfano wa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Sukari ya West Kenya Jaswant Rai.

“Kwamba Wabunge walikuwa waking’ang’ania kumsalimia Bw Rai ni ishara kuwa alikuwa wakitaka kuhongwa ili waandaye ripoti ya kumpendelea mfanyabiashara huyo. Hii ni kinyume cha sheria za bunge. Tangu lini ukaona Jaji wa mahakama akikumbatiana na mshukiwa akiwa kizimbani,?” akauliza Bw Savula.

Joseph Tonui, mbunge wa Kuresoi Kusini allipokana kuwahi kumhonga mwenzake wa Matayos Godfrey Odanga kwa Sh20,000. Picha/ Charles Wasonga

Naye Bw Tonui alikana madai yaliyotolewa na Mbunge wa Matayos Geoffery Odanga mbele ya Kamati hiyo Septemba 19,2018 kwamba yeye (Tonui) alijaribu kumhonga (Odanga) kwa Sh20,000.

“Hayo ni madai ya uwongo. Sina uhusiano wa katibu na Bw Odanga. Na siku hiyo sikuweza kumwona popote katika majengo ya bunge siku hiyo,” akasema.

Naye Bw Gikaria alikana kuwahi kumshawishi Mbunge wa Naivasha Jane Kihara kuangusha ripoti hiyo.

“Kuhusu suala la ripoti ya sukari, sisi kama wabunge kutoka kaunti ya Nakuru hatukuwa na msimamo wa pamoja. Japo binafsi nilipinga ripoti hiyo, wenzangu kutoka kaunti ya Nakuru walikuwa huru kupiga kura walivyopenda,” akasema.

Mnamo Septemba 19, 2018 Bi Kihara alidai mbele ya Kamati hiyo kwamba Bw Gikari alimshawishi kuangusha ripoti hiyo kwa sababu mawaziri wawili wa Jubilee walikuwa wametajwa. Bi Kihara alisema Bw Gikari alimweleza kuwa agizo la kuangusha ripoti hiyo lilikuw limetoka kwa kiongozi wa wengi Aden Duale ambaye alisema “hao ni mawaziri wa Uhuru”.

Kamati hiyo sasa itafanya kikao mnamo Oktoba 3, 2018 kupokea ushahidi kutoka kwa Mbunge Mwakilishi wa Nyeri Bi Rahab Mukami ambaye pia alitajwa na wenzake waliofika mbele ya kamati hiyo mnamo 19/9/2018 na 25/9/2018.

Ni baada ya hapo ambapo kamati hiyo itaandaa ripoti ambayo itawalishwa katika kikao cha bunge lote.