MakalaSiasa

HONGO BUNGENI: Barasa asema Fatuma Gedi alijaribu kumhonga kwa Sh10,000

September 24th, 2018 3 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE waliofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Mamlaka ya Hadhi walitoa kauli zilizokanganya kuhusu iwapo wenzao walihongwa ili kuzima ripoti kuhusu sakata ya sukari nchini.

Ripoti hiyo ambayo iliandaliwa na Kamati ya pamoja ya Kilimo na Biashara ilielekeza kidole cha lawama kwa Waziri wa Fedha Henry Rotich na mwenzake wa Masuala ya Afrika Mashariki Adan Mohamma kwa kuruhusu uingizwaji wa sukari nchini bila kulipiwa ushuru mwaka 2017. Mwingine aliyetajwa na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Felix Koskei ambaye sasa ni balozi wa Kenya nchini India.

Wa kwanza kufika mbele ya kamati hiyo inayochunguza madai hayo ya hongo alikuwa ni Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa  aliyeshikilia kuwa mwenzake Fatuma Gedi (Mbunge Mwakilishi wa Wajir) alijaribu kumhonga kwa Sh10,000 ili aangushe ripoti hiyo.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa akiapishwa na mhudumu wa bunge kabla ya kutoa ushahidi katika kamati ya uchunguzi kuhusu hongo. Picha/ Charles Wasonga

“Alinikaribia na bahasha na kujaribu kunikabidhi ndani ya ukumbi wa bunge. Nilipomuuliza kilichokuwa ndani ya bahasha hiyo, aliniambia kuwa ilikuwa ni Sh10,000 ambazo alitaka nipokee ili niangushe ripoti hiyo. Kitendo chake kilinishangaza ikizingatiwa kuwa Bi Gedi hatoki eneo kunakokuzwa miwa,” akasema.

Bw Barasa alisema Bi Gedi pia alijaribu kumhonga mwenzake wa Sirisia John Waluke ambaye alikuwa ameketi karibu naye lakini Bw Waluke pia alikataa.

Hata hivyo, Mbunge huyo wa chama cha Jubilee alisema hakulenga kuharibu jina la Bi Gedi kwa njia yoyote ile ila lengo lake lilikuwa kulinda heshima na hadhi ya asasi ya bunge.

Mbunge maalum Godfrey Osotsi atoa ushahidi wake mbele ya kamati ya bunge kuhusu madai ya kumumunya mlungula. Picha/ Charles Wasonga

“Sina uadui au uhasama wowote na Bi Gedi kwa sababu anatoka eneo la Kaskazini Mashariki na mimi natoka Magharibi mwa Kenya. Lakini haja yangu kuu ilikuwa ni kulinda maadili maadili na heshima ya bunge,” akasema.

Lakini Bw Waluke alipofika mbele ya kamati hiyo alikana madai kuwa siku hiyo Agosti 9, 2018 alikuwa ameketi karibu na Bw Barasa. Mbunge huyo wa Sirisia pia alisema hakushuhudia mbunge yeyote akijaribu kumhonga.

“Ikiwa Barasa alisema kuwa tulikuwa naye siku hiyo bsi hapo alidanganya. Hii ni kwamba sababu ripoti hiyo ilipokuwa ikijadiliwa nilikuwa nimeketi upande serikali huku Barasa akiketi upande wa upinzani. Na sikuona mtu yeyote akihongwa na hakuna aliyejaribu kunipa pesa zozote,” akasema Bw Waluke.

Mbunge wa Naivasha Jane Kihara alipomhusisha Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale na hongo kwenye uchunguzi. Picha/ Charles Wasonga

Lakini Mbunge huyo alisema habari hizo ziliporipotiwa katika vyombo vya habari alimuuliza Bw Barasa kuhusu suala hilo lakini akamwamba mbunge fulani wa kike wa asili ya Kisomali.

“Aliniambia kuwa Mbunge huyo ‘Oria’ alijaribu kumhonga lakini mimi sikuona mtu yoyote akipatiwa pesa zozote na mimi pia sikupewa hizo. Hata hivyo, nilisikia watu fulani walikuwa wakihongwa,” akasema Bw Waluke.

“Lakini baadaye Bw Barasa aliniambia kuwa Sh10,000 ilikuwa pesa kidogo sana. Na ndipo akaniambia kama zingekuwa Sh100,000 angezichukua,” akasema Mbunge huyo wa Sirisia.

Mbunge wa Matayos Geoffrey Odanga alipodai mbunge wa Kuresoi Kusini Joseph Tonui alijaribu kumhonga kwa Sh20,000. Picha/ Charles Wasonga

Naye Mbunge wa Muhoroni Bw James K’Oyoo alisema kuwa alimsuta Spika wa Bunge Justin Muturi kwa kumnyima nafasi ya kuchangia mjadala kuhusu ripoti ya sakata ya sukari ilhali anatoka katika eneo kunakokuzwa miwa kwa wingi.

“Ni hasira zilinipanda siku hiyo hali iliyozidishwa na madai kuwa wabunge fulani walihongwa ili kuangusha ripoti ya sukari. Hata hivyo, sikushuhudia mbunge yoyote akihongwa,” akasema Bw K’Oyoo huku akiomba msamaha kwa matamshi yake yaliyofasiriwa kama ya kudunisha afisi ya Spika.

Wabunge wengine waliofika mbele ya kamati hiyo waliwa Mbunge Maalum Godfrey Osotsi, Justus Murunga (Matungu), Samuel Atandi (Alego-Usonga) na Simba Arati ambao wote walisema hawakushuhudia kisa chochote cha wenzao kuhongwa.

Mbunge wa Alego-Usonga Samuel Atandi alipokana kuwahi kushuhudia wabunge wakila hongo kuangusha ripoti ya sukari bungeni. Picha/ Charles Wasonga

Lakini jina la kiogozi wa wengi bungeni Aden Duale  lilichipuza katika kikao hicho pale Mbunge wa Naivasha Jane Kihara  alipokudai  kwamba yeye (Duale) ndiye aliyempa Mbunge wa Nakuru Mjini Mashariki David Gikaria kibarua cha “kuwashawishi” wabunge kutoka kaunti ya Nakuru ili waangushe ripoti hiyo.

“Mwenzangu David Gikaria aliniambia kwamba Duale anataka sisi kama wabunge wa Nakuru tuangushe ripoti hiyo kwa sababu iliwahutumu mawaziri wa Uhuru. Nilimwambia kwamba nilichaguliwa na watu wa Naivasha wala sio Uhuru,” Bi Kihara akasema

Lakini  Bi Kihara alifafanua kuwa  Bw Gikaria hakumpa pesa zozote kama hongo japo aliambiwa kuwa kuna baadhi ya wabunge ambao walihongwa.

Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati alipodinda kusema kama aliona wabunge wakila hongo au la. Alisema majibu ya maswali yote yapo kwenye kamera za siri za bunge (CCTV). Picha/ Charles Wasonga

“Kabla ya mjadala kuhusu ripoti kuanza, mwenzangu Rehab Mukami (Mbunge Mwakilishi wa Nyeri) aliniambia kuwa watu walikuwa wakipewa pesa ili waiangushe. Alinieleza Mbunge wa kike aliyevalia mavazi ya buibui ndiye alikuwa akizunguka bungeni akiwapa wabunge pesa…lakini sikumfahamu,” akasema akiongeza kuwa hiyo ndio maana alizungumzia suala hilo katika eneo bunge lake.

Naye Mbunge wa Matayos Mbunge Geoffrey Odanga alidai kuwa mbunge wa Kuresoi Kusini Joseph Tonui Kipkosgei alijaribu kumhonga kwa Sh10,000.

“Nilikuwa nilikishiriki chakula cha mchana pamoja na wageni wanngu wawili pale Mbunge wa Kuresoi Kusini Joseph Kipkosgei aliponiita na kujaribu kunipa bahasha yenye pesa ili niangushe ripoti hiyo. Nilikataa kuchukua pesa hizo ambazo aliniambia zilikuwa Sh20,000,” Bw Odanga akasema.

Mbunge wa Matungu Justus Murunga aliposema kwamba alinukuliwa visivyo na vyombo vya habari. Alisisitiza hakushuhudia hongo bungeni akiongeza kuwa ni mtetezi sugu wa wakulima wa miwa. Picha/ Charles Wasonga

“Mbunge huyo pia alijaribu kumhonga Mbunge wa Butula Geoffrey Onyula lakini akataa. Alisema alitaka ripoti hiyo iangushwe kwa sababu waliotajwa ni watu kutoka eneo anakotoka,” akaongeza.

Spika Muturi alisema kuwa wabunge ambao walitajwa na wenzao mbele ya kamati yake Jumatano waitwa kufika mbele yake Jumanne juma lijalo ili wajitetea kuhusu madai dhidi yao.

Hii ina maana kuwa Mabw Duale, Gikaria na Kipkosgei watafika mbele ya kamati hiyo ili kutoa maelezo kuhusu yale ambayo wanafahamu kuhusu sakata hiyo ya hongo bungeni.