Michezo

Hongo ya ngono kwa polisi yamtupa kichuna jela

September 6th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

Mwanamitindo mmoja, Kira Mayer, amehukumiwa kifungo cha miezi 18 kwa kujaribu kukwepa kutiwa nguvuni kwa kuhonga polisi wawili kwa asali ya ngono.

Kwa mujibu wa gazeti moja nchini Urusi, Mayer alikabiliwa na mashtaka mawili ya kushambulia afisa wa serikali na kukiuka marufuku ya kutoendesha gari barabarani.

Gazeti hilo Komsomolskaya Pravda limeripoti kwamba Mayer alikubali mashtaka ya kushambulia afisa wa polisi baada ya kuamrishwa asimamishe gari lake la aina ya Mercedes jijini Moscow nchini Urusi. Alijaribu kupokonya mmoja wa maafisa hao fomu ya kuandikiwa makosa na katika harakati hizo akamjeruhi.

Mayer alikuwa amepigwa marufuku kuendesha gari baada ya kusababisha ajali na kutoroka eneo la ajali kabla ya maafisa wa polisi kufika hapo. Alipokutana na maafisa wa polisi tena aligundua amevunja sheria iliyomzuia kuendesha gari. Hapo ndipo aliona hongo ya ngono kwa maafisa hao wawili itawazuzua na kuwashawishi kumuachilia.

Inasemekana kwamba Mayer hakutarajia kwamba makosa yake yatafanya asukumwe jela. Alilia hukumu iliposomwa.

Wakili wake alisema atakata rufaa. Anaamini kwamba ushawishi mkubwa mteja wake anao kwenye Instagram utamuepushia kifungo cha jela.