Michezo

Honolulu Marathon yavutia wakimbiaji 27,000

December 8th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKIMBIAJI 27,000 watashiriki mbio za Honolulu Marathon nchini Marekani mnamo Desemba 8, 2018 ambazo Mkenya Joyce Chepkirui ameapa kunyakua taji la wanawake.

Chepkirui alishinda makala ya mwaka 2014 na 2015. Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 30 alimaliza mbio hizi za kilomita 42 katika nafasi ya tatu mwaka 2017.

“Niko sawa sasa na mbio za kilomita 42,” Chepkirui aliambia shirika la habari la Xinhua mnamo Desemba 5. Aliongeza, “Silengi kasi ya juu jijini Honolulu, lakini ushindi. Sina presha. Nahitaji kujitahidi kupata ushindi Honolulu.”

Wapinzani wake wakuu ni Sheila Jerotich, ambaye alimaliza marathon kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola mwaka 2018 katika nafasi ya nne mjini Gold Coast nchini Australia.

Jerotich na Chepkirui hufanya mazoezi pamoja na mshikilizi wa rekodi ya mbio za kilomita 21 Joyciline Jepkosgei, ambaye alipanga kushiriki, lakini jeraha la mguu likamweka nje. Mkenya Vivian Jerono Kiplagat, ambaye ni bingwa wa Buenos Aires Marathon, pia yuko katika orodha ya kinadada watakaoshindania taji Jumapili jioni.

Ezekiel Kemboi, Titus Sang, Charles Cheruiyot, Reuben Kerio, Titus Ekiru, Philip Tarbei, Wilson Chebet na Vincent Yator watapeperusha bendera ya Kenya katika kitengo cha wanaume.