Hosea Kiplagat, mwandani wa zamani wa Mzee Moi, afariki

Hosea Kiplagat, mwandani wa zamani wa Mzee Moi, afariki

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA mwenyekiti mrasimu wa Benki ya Co-operative na mwandani wa karibu wa rais wa zamani marehemu Daniel Moi, Hosea Kiplagat, amefariki.

Kulingana na familia yake, Kiplagat ambaye pia alikuwa mwenyekiti mrasimu wa KANU tawili la Baringo, alifariki Jumamosi asubuhi alipokuwa akikimbizwa katika Nairobi Hospital baada ya kuugua.

Bw Kiplagat alifariki akiwa na umri wa miaka 76. Marehemu alizaliwa katika kijiji cha Cheplambus, tarafa ya Tenges, kaunti ya Baringo.

Alifanya kazi kama askari wa magereza kabla ya kuteuliwa na Rais Moi kuwa mmoja wa washauri wake wakuu katika miaka ya 1980s.

Kiplagat alikuwa mfanyabiashara mashuhuri ambaye aliwekeza katika sekta mbalimbali.

Aliwania kiti cha ubunge cha Baringo ya Kati katika uchaguzi mkuu wa 2007 lakini akashindwa na aliyekuwa Kamishna wa Ardhi Sammy Mwaita.

Lakini mapema mwaka huu masaibu yalianza kumwandama Bw Kiplagat, mahakama ilipotoa idhini kwa Bank of India kupiga mnada mali yake baada ya kampuni yake kufeli kulipa mkopo wa Sh375 milioni.

Kampuni kwa jina Timber Treatment International yenye makao yake makuu mjini Eldoret ilikopesha pesa hizo mnamo Julai 2017.

You can share this post!

Utarukwa 2022, Ruto aonya Raila

Ruto awafokea waliopeleka bandari kavu Naivasha