Habari Mseto

Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kufunguliwa Agosti

May 6th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

HOSPITALI kuu mpya ya kitaifa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta inatarajiwa kufungua milango yake rasmi hapo Agosti.

Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki alisema ujenzi wa hospitali hiyo ni wa kipekee na itaweza kuhudumia wagonjwa wenye maradhi sugu yanayohitaji uchunguzi zaidi.

Waziri huyo aliandamana na mwenzake wa elimu Prof George Magoha na maafisa wakuu wa bodi ya hospitali hiyo.

Alisema ameridhika kuona vifaa vya hali ya juu vilivyoko katika hospitali hiyo akisema ni dhihirisho tosha kuwa hospitali hiyo ni ya kitaifa.

“Nina imani ya kwamba hospitali kuu ya Kenyatta National Hospital, itapunguziwa mzigo ya wagonjwa ambapo wengine wataletwa katika hospitali hii ya Kenyatta University Referal Hospital,” alisema Bi Kariuki.

Alisema ana imani ya kwamba madaktari walio na ujuzi wa hali ya juu wataletwa kwenye hospitali hiyo.

Mitambo ya kisasa ya kukagua wagonjwa katika hospitali hiyo. Picha/ Lawrence Ongaro.

Waziri wa Elimu Prof Magoha alisema hospitali hiyo inalinganishwa na zile za kimataifa kama Afrika Kusini.

“Mimi nimesafiri nchi nyingi za ulimwengu, na ningetaka kuwajulisha kuwa hospitali hii italinganishwa na hizo. Kwa hivyo hakuna haja ya kusafiri nchi ya India kutafuta matibabu huko,” alisema Magoha.

Aliwahimiza wakuu wa hospitali hiyo kuhakikisha vifaa vilivyo wekwa humo vinapata wataalam wa kuvirekebisha vikipata hitilafu.

Mwenyekiti wa bodi ya hospitali hiyo Prof Olive Mugenda, alisema kwa wakati huu maafisa hao wanafanya mikakati kuona ya kwamba kila kitu kipo shwari ili kazi ianze rasmi mwezi Agosti.

Alisema hospitali hiyo itakuwa na vitanda 650 vya wagonjwa ambazo zitajumuisha watu wazima na watoto.

“Tuna imani ya kwamba hospitali hii itahudumia wagonjwa wengi kwa sababu kutakuwa na madaktari wa kutosha,” alisema Prof Mugenda.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dkt Andrew Toro alisema hospitali hiyo itakuwa na kazi nyingi huku likiwa na madaktari wa kutosha.

“Tayari nimepata madaktari 30 waliohitimu ambao watakuwa mstari wa mbele kuhudumia wagonjwa.Kile tunachohitaji kwa sasa ni ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi na wanahabari,” alisema Dkt Toro.