Habari Mseto

Hospitali ya Gatundu yapanda ngazi

December 26th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

HOSPITALI ya Gatundu level 5, itapanda ngazi hadi kiwango cha level 6, kutokana na ongezeko la wagonjwa.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, alisema kulingana na uchunguzi ulofanywa miezi mchache iliyopita lilipatikana ya kwamba wagonjwa ni wengi wanaofurika katika hospitali hiyo.

“Kulingana na jinsi mambo yalivyo idadi kubwa ya wakazi wa Gatundu pia inaongezeka mara dufu. Wagonjwa wengi pia hutoka maeneo ya mbali hata Nairobi na Thika kutafuta matibabu hapa” alisema Dkt Nyoro.

Alisema hata ingawa mgomo wa madaktari na wahudumu wa afya ilikuwa imetisha sekta ya afya, alisema kaunti yake haitaruhusu kazi kusimama kabisa.

“Hata kama ni kutafuta wataalamu wa afya wa kutusaidia kwa muda fulani tutafanya hivyo. Hatuwezi kubali kuona watu wakifariki huku tukiweka mikono yetu nyumba eti hakuna wahudumu wa afya atafuatilia hiyo yote,” alisema gavana huyo.

Alisema hata ingawa kuna matatizo machache ya ukosefu wa maji eneo la Gatundu, ukweli wa mambo ni kwamba kaunti hiyo itatenga sh 600 milioni za kushughulikia shida hiyo.

Aliyasema hayo mjini Gatundu alipozuru huko kuelewa matatizo inayowakumba wakazi wa eneo hilo. Alisema hospitali ya Gatundu ina mitambo wa kisasa wa kufuatia malazi yaliyo kwenye hospitali hiyo.

“Hapo awali wafanyi kazi walizoea kufua malazi ya hospitali hiyo kwa kutumia mikono jambo lililokuwa ni hatari kwa hali yao ya afya,” alisema Dkt Nyoro.

Alikiri wafanyikazi wa kaunti hawajalipwa mishahara ya miezi miwili lakini kaunti yake itafanya wafanyi kazi hao wawe na tabasamu kabla ya kwenda krisimasi hii kwani nao sharti wafurahie sikukuu na wapendwa wao kwa njia ya furaha.